Monday, 25 April 2016

Edward Loure na Tuzo ya Mazingira kutoka Goldman

Mtanzania aliyeshinda tuzo za mazingira Edward Loure
Tanzania Edward Loure kutoka jamii ya wafugaji ya Kimasai ni miongoni mwa watu 6 kutoka mabara mbalimbali duniani aliyepata tuzo ya mazingira inayotolewa na Taasisi ya Mazingira ya Goldman. 

Tuzo hizo zinatolewa kwa wanaharakati wa mazingira katika ngazi za chini kabisa.
Washindi wengine waliopewa tuzo na nchi zao katika mabano ni Leng Ouch (Cambodia), Zuzana Caputova (Slovakia), Luis Jorge Rivera Herrera (Puerto Rico), Destiny Watford (Marekani) na Máxima Acuña wa Peru. Loure amefanya kazi iliyotambuliwa na taasisi ya Goldman kupitia majaji wake. Mtanzania huyo na wenzake wamefanya kazi kuhakikisha jamii zao zinaendeleza uchumi wao na wa taifa kwa kupigania uwepo wa maeneo ya ulishaji mifugo.

Loure ni mfano wa kuigwa kutokana na juhudi zake zilizowezesha kuwepo ekari 200,000 kwa matumizi ya kizazi kijacho. Katika maelezo kuhusu tuzo hizo, Goldman wanasema, Loure ameongoza juhudi za kuwezesha vijiji kupewa hati za umiliki wa ardhi badala ya watu binafsi kaskazini mwa Tanzania; na hivyo kuwezesha usalama wa ekari hizo 200,000.

No comments:

Post a Comment