Sunday 19 June 2016

Hii ndio siri nzito aliyoizungumza Edward Lowasa kuhusu ujio wa TB Joshua nchini baada ya uchaguzi.

Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa amesema hakuridhika na matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, na kwa kulijua hilo, ‘watawala’ walimleta rafiki yake kutoka Nigeria, TB Joshua ili amshawishi akubali matokeo. 

Lowassa alisema baada ya TB Joshua, muhubiri na kiongozi wa Synagogie Church of All Nations, kukaa naye pamoja na viongozi wengine wa Chadema na kumueleza jinsi ‘walivyoporwa’ ushindi, kiongozi huyo wa kidini alichukia na kusitisha azma yake ya kuhudhuria sherehe za kumuapisha Rais John Magufuli.

TB Joshua aliwasili nchini Novemba 3, siku mbili kabla ya kuapishwa kwa Magufuli kuwa Rais, na alienda Ikulu na baadaye nyumbani kwa Lowassa ambaye alitumia muda mwingi wa ziara yake pamoja naye. 

“Walimuita rafiki yangu TB Joshua, wakaenda wakampokea. Alipokelewa na Rais Magufuli, akapelekwa Ikulu akazungumza na Kikwete,” alisema Lowassa. 

“Baadaye akawaambia wamlete kwangu. Kweli akaja nyumbani kwangu, tukazungumza naye. Sitaki kusema mengi sana niliyomwambia, lakini moja, nilimwambia ukikubali yale matokeo ndugu yangu, heshima yako itashuka hapa nchini na duniani kwa ujumla,”alisema. 

Lowassa alisema hayo jana alipokuwa akizungumza katika mahafali ya Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Wafuasi wa Chadema (Chaso) katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam. 

Alisema ni kutokana na msimamo na mazungumzo waliyofanya na TB Joshua ndio yaliyosababisha kiongozi huyo wa kidini maarufu barani Afrika kutohudhuria sherehe hizo za kuapishwa zilizofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

Katika hotuba yake, Lowassa alimpongeza Rais Magufuli kwa jitihada anazozichukua za kujaribu kufufua uchumi wa nchi, lakini akasema hakubaliani na mbinu anazotumia. 

Alisema anafurahia kumsikia Rais Magufuli akiihubiri nchi ya viwanda, lakini hana imani na lugha anazotumia.

“Rafiki zangu nawasikia na nafurahi sana wanasema wanataka kujenga nchi ya viwanda. Natamani nchi hiyo, lakini lugha hiyo sina imani nayo sana,” alisema. 

Alisema haziamini lugha hizo kwa kuwa ni vitu visivyowezekana kutokana na ukweli kuwa viwanda vilivyopo haviwezi kufufuka na kuondoa tatizo la ajira lililopo nchini. 

“Wanasema watafufua viwanda, lakini viwanda vilivyopo vili kuwa analojia sasa hivi mambo yote ni ‘digital’. Hicho kiwanda kitafufuliwaje maana hata madukani spea zake hazipo labda zitengenezwe upya,”alisema. 

Alisema tatizo lililopo kwa sasa nchini ni la ajira na kwamba hata kaulimbiu yao kwenye kampeni ilikuwa ajira kwa kutambua kuwa wapo vijana wengi waliomaliza vyuo, hawana ajira na kwamba eneo kubwa litakaloweza kuwaajiri ni sekta ya kilimo. 

Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, alisema anakubaliana na kauli iliyotolewa na Jenerali Ulimwengu aliyoitoa hivi karibuni kuwa Rais Magufuli ameturudisha nyuma miaka 50, akiponda uamuzi wa Serikali kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja. 

“Uamuzi ule si mzuri na una matatizo makubwa kwa kuwa ni kuwanyima wananchi haki yao muhimu ya kuwasikiliza wawakilishi wao,” alisema.

Akizungumzia elimu, Lowassa alisema wakati Chadema na Ukawa waliposema watatoa elimu bure kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu walikuwa wamejipanga, lakini Serikali imebeba sera hiyo bila kujiandaa.

Aliwapongeza vijana kwa kuwa kiini cha mabadiliko na kusema mpaka sasa akikutana na watoto wadogo wanamsalimia kwa kumwambia “Mabadiliko Lowassa”. 

Alisema vijana walifanya kampeni nzuri na kumwezesha kupata kura nyingi zilizowapa ushindi, lakini wakanyimwa ushindi. 

“Tulishinda vizuri sana lakini hata hizo walizotupa, zinatosha kuwaambia kuwa tuliwapa kazi ya kutosha. Nyie mnajua, wao wanajua na mimi najua,” alisema. 


USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment