Friday, 17 June 2016

Haya ndio maamuzi ya serikali kuhusu kutumia Lugha ya Kiswahili katika mikutano ya kimataifa.

TANZANIA inatarajiwa kuanza kutumia Kiswahili katika mikutano yote ya kimataifa itakayowakilishwa na viongozi wake baada ya serikali kukamilisha kutuma wataalamu watakaotafsiri lugha hiyo kwa watumiaji wa lugha nyingine duniani.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo jana katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Zainabu Vulu (CCM).

Vulu katika swali lake alihoji namna serikali inavyoenzi lugha ya Kiswahili ambayo ilitumika na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuunganisha Taifa na inatumiaje fursa ya kutumika kwa lugha hiyo kimataifa, kuwa ajira kwa Watanzania.

Akifafanua jibu lake, Majaliwa alisema tayari serikali ilishaamua Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kutumika serikalini na hata bungeni na sasa lugha hiyo imekua zaidi na kuwa moja ya lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kwa mujibu wa Majaliwa, tayari duniani kote vyuo vikuu vimeanza kufundisha Kiswahili, hali iliyosababisha kuongezeka kwa mahitaji ya walimu wa kufundisha lugha hiyo kutoka Tanzania.

Kutokana na uhitaji huo, Majaliwa alisema vyuo vikuu karibu vyote nchini, vinafundisha walimu wa lugha hiyo kwa ajili ya kukidhi mahitaji hayo ya kimataifa, lakini pia serikali inajiandaa kupeleka wataalamu wa kutafsiri Kiswahili kwenda katika nchi mbalimbali.

Alisema lengo la serikali kupeleka wataalamu hao katika nchi mbalimbali ni kuwezesha viongozi kutoka Tanzania wanapokwenda katika mikutano ya kimataifa, watumie Kiswahili na wataalamu hao watoe tafsiri kwenda kwenye lugha nyingine za kimataifa.

Alisema kwa sasa Tanzania imeshapeleka walimu wa lugha hiyo Burundi, Rwanda, Uingereza na Ufaransa ambako wanafundisha lugha hiyo na kati ya lugha kubwa za kimataifa, Kiswahili kama si lugha ya sita ni ya nane.

Naye Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima (CCM), alimtaka Waziri Mkuu kuangalia uwezekano wa kuruhusu wabunge kuwa wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mikoa.

Akijibu ombi hilo, alisema wajumbe wa kamati hizo katika wilaya, mikoa na kitaifa, wameainishwa na Sheria ya Usalama wa Taifa kuwa ni wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, ambao ni tofauti na mbunge ambaye ni mwakilishi wa wananchi kisiasa.



Alisema majukumu yao ni kuangalia hali ya usalama kwa undani, lakini sheria hiyo haijamzuia mbunge au mwananchi yeyote, kwenda kutoa taarifa kama ilivyotokea katika mauaji ya hivri karibuni, ambapo kamati hizo kutokana na ushirikiano kutoka kwa wananchi, wahusika wameanza kukamatwa mmoja baada ya mwingine.

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment