Thursday 7 July 2016

Hii ndio kauli ya Rais wa Zanzibar Dk.Shein kuhusu Serikali ya mpito zanzibar.

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema uchaguzi mkuu visiwani humo ulishamalizika na hakuna mpango wa kuwepo kwa serikali ya mpito.

Amesema uchaguzi umekwisha kabla ya mwingine utakaofanyika mwaka 2020; hivyo kazi kubwa inayofanywa sasa ni kusimamia na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Alisema hayo jana wakati akihutubia Baraza la Iddi na kusisitiza kuwa atapambana na watu ambao wamekuwa wakifanya mbinu serikali ishindwe kutekeleza mipango yake.

Alisema wapo watu wamekuwa wakijaribu kufanya mbinu na vituko serikali ishindwe kutekeleza mipango yake, ikiwemo kusimamia ilani ya chama na bajeti ya serikali kwa mwaka 2016/2017.

Dk Shein aliwapongeza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kupitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017, ambayo kazi kubwa itakayofanywa ni kusimamia mapato na kupata fedha za kutekeleza mipango hiyo.

“Wananchi napenda kusema tena kwamba uchaguzi umekwisha na utafanyika mwingine ifikapo mwaka 2020...wanaotaka kuwepo kwa serikali ya mpito wasahau,” alisema.

Alisema hakuna sababu ya kuwepo kwa serikali ya mpito kwa sababu CCM ilishiriki katika uchaguzi wa marudio na kushinda kwa kishindo. 

Aliwataka wananchi kupuuza propaganda zinazotolewa na wapinzani kwa ajili ya kile alichosema ni kuwazubaisha wananchi washindwe kufanya kazi zao vizuri.

Alikemea matukio yanayojitokeza zaidi katika kisiwa cha Pemba, yakiashiria uvunjifu wa amani na utulivu.

Alivitaka vyama vya siasa kufanya kazi zao bila ya kukiuka sheria zilizopo. Alisema vitendo vya chuki na ufisadi ni kinyume na maagizo ya Mungu.

“Nimesikitishwa sana na matukio yote ambayo yamelitia aibu kubwa taifa letu kwani hayaendani na mafunzo tuliyoyapata katika kipindi cha swaumu...tunatakiwa kuacha kujenga kiburi na ufisadi,” alisema.

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment