Sunday, 10 July 2016

Jeshi la Polisi Latoa onyo ili Kwa vyama vya Siasa kuhusu Msaada Katika Shughuli za Kiulinzi.

ONYO limetolewa kwa vyama vya siasa vinavyojaribu kusuguana na Jeshi la Polisi kukumbuka kuwa hilo ni jeshi, ambalo liko tayari kutumia nguvu na rasilimali zote, kuhakikisha raia na mali zao ni salama.

Jeshi hilo pia limesema halihitaji msaada wowote kutoka kwa vyama vya siasa na wakihitaji msaada, wataomba kutoka katika vyombo vingine vya kiusalama.

Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya, baada ya Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), kudai kuandaa vijana kwenda Dodoma kusaidia polisi kuzuia Mkutano Mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika Julai 23 mwaka huu.

“Nawaasa vijana, watoto msisuguane na jeshi, si busara kusuguana na jeshi, fanyeni mambo ambayo nchi itakuwa salama, polisi itatumia nguvu zote pamoja na rasilimali tulizonazo kuhakikisha raia na mali zao wanabaki salama.

“Hakuna suala la kusaidia Jeshi la Polisi au nini, sisi tunajitosheleza wenyewe, kama tutahitaji msaada wowote katika ulinzi basi msaada huo tutauomba kwa vyombo vingine vya ulinzi, ambavyo vina mafunzo kama sisi na si kwa vyama vya siasa,” alionya.

Alisema anatumia neno ‘ole’ kwa watu watakaojaribu kuvuruga amani kwa madai ya kusaidia kuzuia mkutano, kwamba polisi haitasita kuchukua hatua.

Alifafanua kuwa Jeshi la Polisi halijazuia mikutano yote ya kisiasa na kwamba limelazimika kutoa ufafanuzi, kutokana na kuibuka kwa tafsiri tofauti kutoka kwa vyama vya siasa na makundi ya watu, baada ya polisi kutoa tamko Juni 7 mwaka huu la kupigwa marufuku mikutano ya hadhara.

Mssanzya alisema hakuna sehemu yoyote tamko hilo lilipiga marufuku mikutano ya kiutendaji na kiutawala ya vyama vya siasa iliyofanywa kwa mujibu wa kanuni za vyama husika.

“Ndio maana baada ya tamko lile, baadhi ya vyama vimefanya na kupanga kufanya mikutano ya kiutendaji na kiutawala bila kuingiliwa au kuzuiwa na Jeshi la Polisi,” alisema Mssanzya akitolea mfano mkutano wa Bavicha kuzungumza na vyombo vya habari Julai 3, mwaka huu.

Alisema shughuli ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Chadema (Chaso) iliyopanga kufanyika Dodoma na ule wa chama cha ACT Wazalendo, ilizuiliwa kwa sababu ujumbe uliolengwa katika shughuli hizo, ulikuwa wa uchochezi na haikuwa mikutano ya kiutendaji au kiutawala.

Hata hivyo alisema pamoja na vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano hiyo ya ndani, bado jeshi hilo lina mamlaka ya kuzuia pale itakapobainika ina lengo la kuhamasisha uchochezi au kuharibu amani na utulivu.

Alitoa mwito kwa wananchi wote na vyama vya siasa, kuheshimu sheria za nchi na kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zake unaendelea kuimarika.

No comments:

Post a Comment