Friday 19 August 2016

Hizi ndio Sababu za Kutumbuliwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Felix Ntebenda.

Daudi Felix Ntibenda jana asubuhi alikuwa na majukumu ya kufungua mikutano miwili na kufanya shughuli nyingine kwa nafasi yake ya mkuu wa Mkoa wa Arusha, lakini hakuweza kuyatimiza kikamilifu majukumu hayo kwa kuwa Rais John Magufuli alikuwa na mawazo tofauti na mipango yake.


Habari za uhakika kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa zinasema kuwa kabla ya kuibuka kwa taarifa za kutenguliwa kwake, Ntibenda alikuwa na mazungumzo na Gambo ofisini kwake.

Haikujulikana mara moja mambo waliyozungumza wawili hao, ingawa tangu Ntibenda ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kumekuwa na utulivu wa kisiasa.

Ntibenda alikuwa kwenye mzozo na viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ambao walikuwa wakimlalamikia kuingilia majukumu ya jumuiya hiyo.

Mwenyekiti wa UVCCM wa mkoa, Lengai ole Sabaya aliwaambia waandishi wa habari mapema wiki iliyopita wakati akisoma maazimo ya kamati ya utekelezaji, kuwa mkuu huyo anakwamisha utendaji wao.

Katika taarifa hiyo UVCCM ilisema kitendo cha Ntibenda kuingilia kati sakata la mikataba ya wapangaji katika maduka ya jumuiya hiyo ni kuwakwamisha.

Baadaye kundi la viongozi hao wa UVCCM pia lilidaiwa kuandika barua ya kumlalamikia Ntibenda kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake.

Hata hivyo, Ntibenda alikanusha tuhuma zote za UVCCM kumtetea mmoja wa wapangaji na kusema anasikitishwa na madai hayo dhidi yake.


Kuondolewa Ntibenda
Lakini hali ilikuwa tofauti kwa mbunge wa Arusha, Godbless Lema aliyesema anaona vurugu zikirudi na kwamba uteuzi wa Gambo ni kama mkakati wa kuhakikisha wapinzani wanasambaratishwa mkoani Arusha ambako ni moja ya ngome za Chadema.

Lema, ambaye amekuwa katika mgogoro na Gambo katika siku za karibuni, alisema kada huyo ameteuliwa ili kuidhibiti Chadema, jambo ambalo chama hicho hakitakubali.

“Hivi karibuni nilimwambia mkuu wa mkoa Ntibenda kuna watu wanakutafuta, sasa wamefanikiwa. Lakini mimi naona Arusha ijayo itakuwa na vurugu tofauti na utulivu uliopo sasa,” alisema.

Hata hivyo, alisema Chadema imejipanga kuendelea kufanya siasa za kistaarabu na kamwe haitakubali kuhujumiwa na mtu yeyote yule.

Alipotafutwa jana asubuhi, Gambo alisema hana cha kuzungumza na kwamba hakuwa na taarifa rasmi.

Gambo, ambaye jana alishiriki mkutano wa Tasaf kwa nafasi yake ya mkuu wa Wilaya ya Arusha na baadaye kuondoka, alisema alikuwa hajapata taarifa rasmi.

Hata hivyo, akiwa kwenye mkutano baadhi ya wakuu wa mkoa na wakuu wa wilaya za mikoa ya Kanda ya Kaskazini, walimpongeza kwa uteuzi huo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega alisema alipata taarifa za uteuzi huo jana asubuhi na alipata maelekezo kuwa Gambo anatakiwa Dar es Salaam.

“Nilipata taarifa rasmi ya uteuzi wake na tayari tulikuwa naye hapa ofisini ili kuweka taratibu za kwenda kuapishwa,” alisema.

Alisema Gambo atarejea Jumamosi na atapokewa na wafanyakazi na baadaye kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Ngorongoro

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment