Wednesday, 18 January 2017

AUDIO:Sikiliza kauli ya Freeman Mbowe kuhusu kitendo cha Lowasa kukamatwa na polisi.


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amelaani kitendo cha polisi wa Mkoa wa Geita kumshikilia kwa zaidi ya saa tatu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alipokuwa njiani kwenda kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo Kata ya Nkome wilayani Geita juzi.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limesema halikumkamata mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema, badala yake lilimwita kituoni kwa ajili ya kuhakikisha usalama wake na wa wananchi waliokuwa wamemzunguka.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, Mbowe alisema huo ni mwendelezo wa ghiliba, hila na unyanyasaji unaofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani kwa lengo la kuinufaisha CCM.

Akifungua kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Chadema, Mbowe alipinga maelezo ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Mponjoli  Mwabulambo kuwa walimshikilia Lowassa kwa usalama wake, akihoji sababu za kuchukua maelezo yake.

“Tumesikia maelezo yaliyotolewa na kamanda wa Polisi kuwa Lowassa alishikiliwa kwa usalama wake. Unayemlinda usalama wake unamwandikisha maelezo?” alihoji Mbowe.

 Alisema lengo la polisi, lilikuwa ni kuhakikisha kuwa Lowassa hafiki na kuhutubia mkutano wa kampeni.

Akizungumzia kuzuiwa kwa shughuli za kisiasa nchini, kiongozi huyo alilitaka jeshi la polisi kuacha umma uonyeshe mapenzi yao kwa viongozi wanaowapenda.

“Nchi hii inastahili kuongozwa katika misingi ya sheria badala ya chuki, ghiliba na ukandamizaji kama tunavyoshuhudia hivi sasa,” alisema.

Alisema ukimya na upole wa vyama vya siasa kunyamazia ukandamizwaji, usichukuliwe kuwa ni udhaifu bali ni busara inayolenga kuepusha jamii na mgawanyiko kiitikadi.

Lowassa aliyegombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa tiketi ya Chadema baada ya kujiengua kutoka CCM, alishikiliwa mjini Geita kuanzia saa 9:30 alasiri hadi saa 12:52 jioni baada ya kusimama na kuwasalimia wananchi waliojitokeza alipokuwa eneo la soko kuu

Msikilize hapa.

No comments:

Post a Comment