Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe ameachiwa huru Septemba 21, 2017 toka amekamatwa na polisi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Septemba 20 na kupelekwa Dodoma kwa ajili ya mahojiano na kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Zitto Kabwe ambaye jana aliweza kukutana na Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na kufanya mahojiano nao amesema kuwa kwa upande wake yeye ametimiza wajibu wake hivyo sasa kazi imebaki kwenye Kamati husika kupima maelezo yake na kile anachotuhumiwa na kufanya maamuzi, lakini pia amesema anaamini Kamati hiyo itafanya maamuzi kwa haki na bila ya kuwa na woga wala hofu.
"Nipo huru baada ya masaa 24 tangu nikamatwe na polisi Uwanja wa Ndege Dar es Salaam na kuletwa Dodoma kwa gari. Nimekutana na Kamati ya Bunge ya Kinga na Haki na kuhojiwa. Nimetoa maelezo yangu yenye lengo la kulinda Uhuru wa maoni na kulinda hadhi ya Bunge kama mhimili wa dola dhidi ya kuingiliwa na Serikali. Nimetimiza wajibu wangu. Mpira sasa upo kwenye Kamati natumai wataamua kwa haki na bila woga na hofu" alisema Zitto Kabwe
Zitto Kabwe alikamatwa na jeshi la polisi kwa amri ya Katibu wa Bunge Dr. Thomas D. Kashililah na kuweza kusafirishwa kutoka Dar es Salaam mbaka Dodoma chini ya ulinzi wa jeshi la polisi kwa lengo la kuhojiwa na kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kutokana na kauli zake alizowahi kutoa kupitia mitandao ya kijamii dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Bunge.
No comments:
Post a Comment