Kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohammed Issa ‘Banka’, ameonekana kuwa gumzo kwenye kambi ya Simba kuelekea mechi yao ya kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Banka anayecheza nafasi ya kiungo namba sita, kwenye mechi iliyopita ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga iliyomalizika kwa suluhu, alionekana kumiliki safu hiyo ya kiungo mbele ya nyota Thabani Kamusoko, Pius Busitwa na Said Makapu mchezo uliopigwa uwanjani hapo.
Simba na Mtibwa kesho zinacheza mechi ya ligi kuu ambayo inaweza kutoa jibu la timu itakayokaa kileleni mwa ligi hiyo kwani zote zina pointi 11, Simba ikiongoza ikifuatiwa na Mtibwa.
Ndani ya benchi la ufundi la Simba, wamesema watamtupia macho Banka kutokana na namna alivyocheza dhidi ya Yanga ili kuhakikisha hawazuii kupata ushindi.
Alisema wanajua Banka ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi zilizonyooka na kukaba kwa wakati mmoja, hivyo tayari benchi lao limetengeneza mbinu za kukabiliana naye.
“Mchezaji tunayemhofia Mtibwa ni yule dogo mwenye rasta (Banka) ambaye aliitwa Taifa Stars hivi karibuni na kama unakumbuka mechi dhidi ya Yanga, yeye ndiye aliyewatibulia mipango.
“Banka ana uwezo wa kuchezesha timu na kuzuia mashambulizi na kuna wakati anatibua kabisa kwa kucheza rafu ili kuwatisha wachezaji wa timu pinzani,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Banka kuzungumzia kuhofiwa kwake, alisema: “Tutajuana humohumo uwanjani tutakapokutana, wao si wamesajili wachezaji wazuri, tutaonana siku hiyo.
“Mimi simuhofii mchezaji yeyote na mechi hizo kubwa za Simba na Yanga ndiyo ninazozitaka mimi kwani ninaongeza uwezo wa kujiamini zaidi, Simba wajiandae.”
No comments:
Post a Comment