Monday 14 March 2016

TOTAL yamuhakikishia Rais MAGUFULI kujenga bomba la mafuta kwa wakati

 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki, Javier Rielo Ikulu jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki JAVIER RIELO  amemuhakikishia Rais Dr. JOHN MAGUFULI, kuwa kampuni hiyo itaanza ujenzi wa mradi wa bomba la kusafirisha Mafuta kutoka nchini UGANDA hadi bandari ya TANGA haraka, kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo.


RIELO ametoa ahadi hiyo leo alipofanya mazungumzo na Rais MAGUFULI Ikulu Jijini DSM, ambapo amemueleza Rais MAGUFULI kuwa Kampuni yake inatarajia kutumia dola za kimarekani bilioni 4 ambazo tayari zimeshaandaliwa.

Mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 1,410 ambalo litasafirisha mafuta ghafi kutoka ziwa ALBERT nchini UGANDA hadi Bandari ya TANGA na unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.

Rais MAGUFULI ameukaribisha uwekezaji huo mkubwa kwa Tanzania, na kuitaka kampuni hiyo kuharakisha mchakato wa kuanza kwa mradi, na kushauri muda wa miaka mitatu uliopangwa kuukamilisha mradi huo upunguzwe, ili manufaa yake yaanze kupatikana mapema.

Naye Waziri wa Nishati na Madini Prof. SOSPETER MUHONGO, amesema Wizara yake ipo tayari kuhakikisha mradi huo unafanikiwa, na itatoa ushirikiano wa kutosha kuharakisha utekelezaji wake.

No comments:

Post a Comment