MAGARI 213 yanafuatiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya
kubainika yameingizwa nchini bila kulipiwa kodi na watu binafsi pamoja
na taasisi mbalimbali zikiwemo za dini. Miongoni mwa magari hayo, yamo
yaliyoingizwa kwa misamaha ya Kituo cha Uwekezaji (TIC) ambayo
(misamaha) imetajwa kutumika isivyo.
Mamlaka imesema inafuatilia kuhakikisha wahusika sanjari na
waliosaidia ukwepaji huo wa kodi, wanachukuliwa hatua. TRA imetaja
majina na taasisi zinazohusika na uingizaji magari hayo, kupitia
matangazo kwa vyombo vya habari na imetoa siku nne wajitokeze kulipia
ushuru kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa.
Ukaguzi uliofanywa na mamlaka, ndiyo umebaini kuwepo kwa magari hayo
yaliyoingizwa nchini na kusajiliwa bila kufuata taratibu za forodha
hivyo kuyafanya yamilikiwe bila kulipiwa kodi stahili. Orodha ya magari
213 na namba za usajili, mmiliki na aina ya gari imetolewa katika vyombo
vya habari na mamlaka hiyo imewataka wahusika wajitokeze haraka kulipia
gharama hizo.
Baadhi ya kampuni, taasisi na watu binafsi, wameingiza magari zaidi
ya moja. Miongoni mwa taasisi zilizotajwa kwenye orodha hiyo zenye
magari zaidi ya moja ni JM Hauliers Limited (26), Al-Jabri Co Ltd (16)
na Kampuni ya Dhandho Road Hawlage iliyoingiza 18.
Kampuni nyingine na idadi ya magari yaliyoingizwa kwenye mabano ni
Bamboo Rock Limited (7) na Dayosisi ya Musoma, ambayo hata hivyo
haikufafanuliwa ni ya madhehebu gani ya dini, imeingiza magari manane.
Wengine ni Fai Limited (3), Nam Transport Company (6), Neni Enterprises
(2) na Relief Partner International yenye magari matatu.
Kwa upande wa watu binafsi wenye magari zaidi ya moja yaliyoingizwa
bila kulipia ushuru ni pamoja na Aloyce Kajijira (6), Mohamed Masoud
(5), Mwesige Rwiza (5), Nassor Zakaria (3), Rumishaeli Shoo (3), Ruwaida
Ally (4) Simon Mehi (2), Yahya Hilal (5) na Zahor Issa mwenye magari
matatu.
Wapewa siku nne Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkurugenzi
wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo
aliwataka wamiliki wa magari yaliyoorodheshwa kufika katika ofisi zilizo
karibu, wafanyiwe uhakiki walipe ushuru stahiki kabla ya Machi 12 mwaka
huu.
Alisema baada ya tarehe hiyo, TRA itachukua hatua ya kufuatilia
magari hayo na kuyakamata. Alisema ufuatiliaji wa magari yaliyoingizwa
nchini bila kulipiwa ushuru ni endelevu. Waliouziwa matatani
Akizungumzia watakaokuwa wameuziwa magari hayo bila kufahamu kama
yalitolewa bila kulipiwa kodi stahili, Kayombo alisema pia wanatakiwa
kujitokeza.
Alisema walioyanunua magari hayo, ambayo namba zake zimeoneshwa,
wanapaswa kujitokeza wapigiwe hesabu, walipe kiasi kinachodaiwa na
mamlaka. Kwa mujibu wa Kayombo, watakapofika katika ofisi za TRA,
zitafanyika taratibu kuangali jinsi ya kulipa, kwani yapo magari ambayo
hayakulipiwa kabisa au yamelipiwa kidogo kutokana na kufanya udanganyifu
katika malipo. Waliosaidia ukwepaji kodi Hata hivyo, Kayombo alisema
baada ya kulipa gharama hizo, hatua nyingine zitachukuliwa.
Hatua hizo za kisheria, zitahusu waliopitisha magari hayo na
waliosaidia katika kufanya udanganyifu wa kulipa kodi stahiki kwa magari
hayo. Jipu lingine Kubainika kwa magari hayo ni mwendelezo wa TRA,
kudhibiti ukwepaji kodi baada ya hivi karibuni, kubaini waliokwepa kodi
kwa kupitisha kontena kwa njia ya udanganyifu.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Philip Mpango hivi karibuni alikaririwa
akisema serikali haitafumbia macho watu watakaobainika kutumia TRA kama
pango la kujinufaisha kiuchumi. Dk Mpango alieleza kukerwa na vitendo
vya ubadhirifu vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo ya
kodi wasio waaminifu.
Taarifa za hivi karibuni zinaonesha, TRA katika kukabiliana na
wakwepa kodi, imekusanya Sh bilioni 11.8 kutoka kwa wafanyabiashara
waliokuwa wameondosha makasha yao katika Bandari Kavu kinyume na
taratibu za forodha.
Kaimu Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata alisema hivi karibuni kwamba,
makusanyo hayo yanajumuisha Sh bilioni 5.3 ambazo zimetolewa na kampuni
na wafanyabiashara 19, ambao awali hawakulipa kodi za kontena zao na
wengine 19 ambao wamelipia sehemu ya kodi ya kontena zao.
Wednesday 9 March 2016
Wamiliki wa magari 213 kutumbuliwa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment