Monday, 25 April 2016

Magazeti:Bajeti ya Waziri Mkuu kupitishwa bila Ukawa

 
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema Ijumaa kuwa wabunge wa upinzani watakuwa wanaingia kwenye Ukumbi wa Bunge, lakini hawatachangia vikao vya bajeti mpaka pale hoja zao zitakapojibiwa.

Mwenyekiti huyo wa Chadema na Mbunge wa Hai (Chadema), alizitaja hoja hizo kuwa Serikali ya Awamu ya Tano kufanya kazi bila kuwa na mwongozo wa utendaji kazi kwa wizara mbalimbali, kuvunjwa kwa Katiba na sheria za nchi pamoja na kupokwa uhuru na madaraka ya mhimili wa Bunge kutokana kuzuiwa kwa matangazo ya moja kwa moja (live) ya vikao vya Bunge.
Licha ya upinzani kususa, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alisema vikao vya Bunge vitaendelea kama vilivyopangwa na kwamba leo watamalizia mjadala wa hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2016/17 iliyowasilishwa bungeni Ijumaa.
Chenge alisema hotuba hiyo itajadiliwa kwa siku mbili (Ijumaa na leo), kabla ya wabunge kuamua kuipitisha ama kutoipitisha leo jioni.
Chenge ambaye aliongoza kikao cha Bunge Ijumaa jioni, pia aliishauri Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iende mahakamani kupatiwa msaada wa kisheria akieleza kuwa hoja zao zilikuwa na tuhuma nzito kwa serikali.

MAMBO MUHIMU:

Tume Dawa za Kulevya
Katika mwaka wa fedha 2016/17, Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, alisema serikali itakamilisha utaratibu wa kuanzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulenya ili kuongeza ufanisi.
Alisema mamlaka hiyo itashirikiana na Jeshi la Polisi kubaini mtandao wa wahalifu ndani na nje ya nchi wanaojihusisha na uingizaji wa dawa za kulevya na kuwafikisha wahusika mahakamani.
TUME YA UCHAGUZI
Majaliwa pia aliiagiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya tathmini ya kina kubaini sababu zilizofanya wapiga kura zaidi ya milioni saba waliojiandikisha kupiga kura, kutoitumia haki yao kikatiba.
Alisema itasaidia kuboresha chaguzi zijazo kwa kuwa wananchi wana wajibu wa kutumia haki yao ya msingi kuchagua viongozi wanaowataka.
Aliongeza kuwa tathmini itasaidia kubaini iwapo kuna vikwazo vinavyowazuia baadhi ya watu kupiga kura ili viondolewe kukuza demokrasia nchini.
"Idadi ya wapigakura walioandikishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 ilikuwa 23,161,440 sawa na asilimia 96.9 ya makadirio. Waliopiga kura ni 15,596,110 sawa na asilimia 67.3 ya waliojiandikisha.
Naiagiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya tathmini ya kina kubaini sababu zilizofanya zaidi ya watu milioni saba kutotumia haki yao ya kikatiba," alisema Majaliwa.
DENI MIFUKO YA JAMII
Majaliwa pia, alisema serikali inaendelea kulipa deni la Sh. bilioni 840.4 linalotokana na miradi ya serikali iliyogharamiwa na Mifuko ya GEPF, LAPF, NHIF, NSSF na PPF, huku akieleza kuwa kwa sasa ni asilimia 6.5 tu ya Watanzania wanaofikiwa na huduma za Hifadhi za Jamii.
ATOA AGIZO HALMASHAURI
Waziri Mkuu pia aliwaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi waliokamata mbao ndani ya halmashauri zao kuzitumia 
kutengeneza madawati na siyo kuzipiga mnada.
Alisema Suma JKT na Magereza wameanza kazi ya kutengeneza madawati 80,000 yatakayotolewa kwa majimbo yote (kila jimbo madawati 300) kutokana na Sh. bilioni sita zilizookolewa na uongozi wa Bunge kwa kubana matumizi.
RUSHWA KUBWA 10
Kadhalika, Majaliwa alisema serikali itaendelea kuchunguza tuhuma 3,444 zilizopo na mpya zitakazojitokeza na kukamilisha uchunguzi wa tuhuma 10 za rushwa kubwa.

Na Nipashe

No comments:

Post a Comment