Monday 2 May 2016

Madaktari bingwa wa upasuaji muhimbili na bugando wavuka lengo katika upasuaji watoto wenye vichwa vikubwa

Mkurugenzi wa taasisi ya Mifupa ya Moi, Dkt. Othman Kiloloma
Jopo la Madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili Moi, kwa kushirikiana na Hospitali ya rufaa ya Bugando imevuka lengo la upasuaji watoto 50 baada ya kufanya upasuaji watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi 55 mkoani Mwanza.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Mwanza, Mkurugenzi wa taasisi ya Mifupa ya Moi, Dkt. Othman Kiloloma,amesema zoezi hilo limefanyika kwa mafankio makubwa na watoto wote waliofanyiwa upasuaji wanaendelea vizuri.

Dkt. Kiloloma amesema kuwa wametumia siku nne katika kufanya upasuaji huo ambapo waliweza kufanya kwa watoto 55 lakini waliweza kuwaona wagonjwa wa nje wapatao 65.

Nae Kaimu Mganga Mkuu wa idara ya upasuaji katika hospitali ya rufaa ya Bugando Dkt. Gared Majaja,amewataka wakazi wa Mkoa wa mwanza kufahamu kuwa matibabu hayo ya watoto vichwa kujaa maji na migongo wazi yataendelea kupatika katika hospitali hiyo.

Upasuaji wa watoto hao ambao umegharamiwa na taasisi ya GSM, umetoa ahueni kwa kina mama ambao wanasema kuwa walikuwa wanapata tabu kwenda mpaka jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata matibabu.

Wazazi hao licha ya kuomba kuongezewa madaktari bingwa wa magonjwa hayo hospitalini hapo wametoa wito kwa wazazi wenzao ambao wamewaficha watoto wenye matatizo hayo nyumbani kwa kuona aibu watumie fursa hiyo kwenda hospitali hapo kwani matatizo hayo yanatibika.

No comments:

Post a Comment