Sunday 24 April 2016

Magazetini:Kamati ya Bunge ya PAC kuchunguza Lugumi mwezi mmoja



KAMATI ndogo ya wajumbe tisa iliyoundwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) , imepewa mwezi mmoja kufanya kazi ya uchunguzi kuhusu hoja zote ambazo kamati hiyo haikuridhishwa na majibu yaliyotolewa na maofisa wa juu wa Jeshi la Polisi kuhusu Mkataba wa Lugumi Enterprises na kuleta taarifa itakayowasilishwa bungeni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana bungeni mbele ya kamati hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kamati kutoridhishwa na majibu au hoja mbalimbali zilizotolewa na wahojiwa.
Kamati hiyo ndogo ina wajumbe wanne wa upinzani na watano wa CCM, na inaongozwa na Mwenyekiti, mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM), wajumbe wengine ni mbunge wa Malinyi, Dk Haji Mponda (CCM), mbunge wa Dimani, Hafidhi Tahir (CCM).
Wengine ni mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk (CUF), mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM), mbunge wa Viti Maalum, Tunza Malapo (Chadema), mbunge wa Same Magharibi, Naghenjwaeli Kaboyoka (Chadema) na mbunge wa Viti Maalum, Khadija Ally (CUF).
“Watafanya kila kitu ikiwa ni pamoja na kukagua hizo mashine, watafanya kazi kwa siri na baada ya muda tuliowapa kuisha watatuletea ripoti na sisi tutaiandika na kuwasilisha bungeni,” alisema Hilaly.
Na habari leo

No comments:

Post a Comment