Thursday 21 April 2016

Mkubwa yazidi kuibuka Mkoani shinyanga idadi ya watumishi hewa yazidi kuongezeka kutoka 45 hadi 226



 
Rais John Magufuli ameendelea kumng’ang’ania aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango baada ya kusema idadi ya watumishi hewa katika mkoa huo imeongezeka kutoka 45 hadi 226.

Aprili 11, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Kilango kwa kosa la kutangaza kuwa mkoa huo hauna watumishi hewa, lakini ikabainika baada ya Ikulu kufanya uchunguzi wake kuwa kulikuwa na watumishi hewa 45.
Akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa Daraja la Nyerere Kigamboni, Rais Magufuli alisema amekuwa habahatishi kila anapokuwa akichukua uamuzi wa kutumbua jipu.
Alitoa kauli hiyo dakika chache baada kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe na kusema hatakuwa na mzaha katika utumbuaji wa jipu.
Alisema Watanzania wameteseka sana hivyo wanatakiwa kutumikiwa.
Huku akishangiliwa na maelfu ya wakazi waliokuwa eneo hilo, Rais Magufuli alikumbushia msimamo wake kuhusu Shinyanga akieleza kuwa hadi leo (juzi) kuna wafanyakazi hewa 226, mahali ambako walisema wafanyakazi ni sifuri, hivyo kuwaomba viongozi ambao wanataka kufanya kazi na Serikali yake wajipange kuyaondoa mabaya yaliyo kwenye maeneo yao akisema wananchi wameteseka mno.
watumishi hewa 71 Dar
Jana, akizungumzia suala hilo la watumishi hewa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwaagiza wakuu wa wilaya za Temeke, Kinondoni na Ilala kusimamisha shughuli zao kwa muda ili kulivalia njuga suala la watumishi hewa kwani bado hajaridhika na watu 71 waliopatikana hadi sasa.
Akizungumza wakati akizindua kampeni ya upasuaji watoto wenye tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), Makonda alisema tayari watumishi hewa 34 katika Wilaya ya Kinondoni wameshafunguliwa jalada.
“Nalipongeza jeshi la polisi kwa kumkamata mtu mmoja ambaye alikuwa anajipatia mshahara kwa njia ya udanganyifu, mpaka sasa yupo mikononi mwa vyombo vya sheria kwa ajili ya hatua anazostahili kuchukuliwa,” alisema.
Makonda alisema Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa yenye watumishi wengi wajanja hivyo idadi ya walio hewa aliyonayo kwa sasa hawezi kuitangaza mpaka itakapokamilika, huku akitoa maagizo makuu matatu.
“Wengi wanaonekana wapo kazini, kumbe wanafanya shughuli nyingine, mwisho wa siku wanajiingizia kipato, nikaomba kuongezewa muda mbele ya Waziri (George) Simbachawene (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi), kadri tunavyoendelea idadi inazidi kuongezeka, tumeona ni vyema kuujulisha umma hatua ambazo tumeanza kuzifanya,” alisema.
Alisema ameiomba Utumishi kumpatia utaalamu zaidi ili wajanja wanaopenya wapate nafasi ya kuwabaini mapema.     

No comments:

Post a Comment