RAIS wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein amewaambia wafanyakazi kwamba ahadi yake ya kuongeza kima cha chini cha mshahara ipo pale pale na itatekelezwa katika kipindi cha mwaka wa kwanza akiwa madarakani
.
Aidha, amewataka watumishi wa serikali kufanya kazi kwa ufanisi na kuyafikia malengo yaliyokusudiwa huku akiwataka kuacha kuzigeuza ofisi za serikali kuwa sehemu ya majukwaa ya kisiasa.
Alisema uchaguzi umekwisha na kazi kubwa iliyopo mbele inayoikabili serikali kwa wananchi wake wa Zanzibar ni kuleta ufanisi na kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Dk Shein alisema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa serikali pamoja na wa sekta binafsi katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani kwenye Hoteli ya Bwawani ambazo zilihudhuriwa na mamia ya wafanyakazi.
Aidha, aliwaambia wafanyakazi nchini kwamba ahadi yake ya kuongeza kima cha chini cha mshahara kutoka Sh 150,000 hadi 300,000 ipo pale pale na itatekelezwa katika kipindi cha mwaka wa kwanza akiwa madarakani.
Alisema wapo waliobeza na wapo waliodharau na wengine kuguna wakidhihaki kauli yake ya kuimarisha maslahi ya wafanyakazi na kupandisha kiwango cha mshahara ambayo aliitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.
“Niliahidi kuongeza kiwango cha chini cha mshahara kutoka shilingi 150,000 hadi kufikia shilingi 300,000 katika kipindi cha mwaka wa kwanza nikiingia madarakani napenda kusisitiza kwamba ahadi hiyo ipo pale pale na itatekelezwa kwa vitendo na huo sio mchezo wa kuigiza kama wengine walivyokuwa wakisema,” alifafanua.
Alisema mabadiliko ya mishahara kutoka katika kima cha chini yatafanyika na kutangazwa katika bajeti ya serikali mwezi ujao na wizara husika na kuwataka wafanyakazi wa serikali kuondoa hofu na wasiwasi katika hilo.
Alisema juhudi kubwa zinafanywa katika kuimarisha na kuongeza ajira serikalini pamoja na mabadiliko makubwa yamefanyika katika kipindi cha miaka mitano ikiwemo kuimarishwa kwa sekta binafsi na uwekezaji.
Kwa mfano, alisema katika kipindi cha miaka mitano jumla ya ajira 5,370 zimepatikana serikalini wakati sekta binafsi ikiwemo katika hoteli za kitalii ajira 25,000, na kazi kubwa iliyopo sasa kuimarisha chuo cha utalii ili kutoa wahitimu wenye sifa na vigezo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi pamoja na Jumuiya ya Waajiri Tayari wamefikia hatua nzuri ya kutekeleza mambo muhimu ambayo wamekubaliana kwa ajili ya kuleta ufanisi sehemu za kazi.
“Tumepiga hatua kubwa katika kutekeleza mambo ya msingi ambayo yamefikiwa katika mazungumzo ya pamoja na shirikisho la vyama huru na jumuiya ya waajiri yakiwa na lengo la kuleta ufanisi katika sehemu za kazi,” alieleza.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Zanzibar, Khamis Mussa alisema serikali chini ya Dk Shein imepiga hatua kubwa kwa kujenga ushirikiano mzuri na shirikisho hilo katika kujadiliana pamoja kwa lengo la kuondosha migogoro sehemu za kazi.
Alisema jumla ya mambo 10 yamezungumzwa kwa pamoja katika majadiliano ya kuleta ufanisi wa kazi ambayo serikali imeyatekeleza mambo manane ikiwemo ahadi ya kukutana na wafanyakazi na viongozi wa vyama vya wafanyakazi kwa ajili ya kuzipatia ufumbuzi changamoto ziliopo.
“Tunakupongeza kwa dhati Rais Shein kwa sababu mambo ya msingi tuliyokubaliana kuyapatia ufumbuzi kati ya kumi, manane umeyatekeleza kwa vitendo,” alisema Mussa.
No comments:
Post a Comment