Monday 30 May 2016

Kitengo cha usalama barabarani chafanikiwa kukusanya kiasi hiki cha pesa.

Jeshi la polisi Kanda maalum ya Dar es salaam kupitia kikosi chake cha Usalama barabani Limefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milion 548.16, ikiwa ni tozo kutokana makosa mbalimbali  ya barabarani yaliyofanywa na madereva.

Kiwango hicho cha fedha ni kutokana na makosa 18,272 yaliyokamatwa kwa muda wa siku kumi zilizopita kwenye wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni, huku idadi ya magari yaliyokamatwa yakiwa ni 14, 788, pikipiki 3,484, dala dala 3,520 na magari mengine binafsi na malori yakiwa 11,268

Hayo yamebainishwa leo na kamanda wa polisi wa kanda maalum ya Dar es salaam Kamishna SIMON SIRO Wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa kiasi hicho cha fedha kimeingia serikalini.

Katika hatua nyingine Jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata vijana 15 wanaodaiwa kujihusisha na makundi ya kihalifu maarufu kama Panya road, baada ya kuendesha msako mkali wa kutafuta wahalifu wa makosa mbalimbali kwenye maeneo ya kivule Nyang’andu na Vingunguti Mtakuja.

Kutokana na kuongezeka kwa matukio ya baadhi ya Vijana kujiingiza kwenye makundi ya kihalifu, Kamishna Simon Siro amewataka wazazi na walezi kuwa karibu kufuatilia mienendo ya watoto wao, sambamba na kuitaka jamii kurejesha vikundi vya ulinzi shirikishi.

Kamanda huyo pia amewaeleza waandishi wa habari kuwa katika misako mbalimbali iliyofanywa na jeshi hilo, imefanikiwa pia kukamata bastola na risasi ambazo zilikuwa zikitumika kwenye matukio ya uhalifu kwenye maeneo tofauti ya kanda maalum ya Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment