Thursday, 12 May 2016

Kumbe Tanzania mpaka sasa bado haina sheria ya ujenzi wa majengo.

 
Serikali ya Tanzania mpaka sasa haina sheria ya majenzi yaani Building Act, hali inayofanya kukosekana udhibiti kwa wataalam wa ujenzi wa majengo kwa kuwapa vigezo, miongozo na utaratibu wa namna ambavyo majengo bora yanapaswa kujengwa.

Hatua hiyo inakwamisha ufuatiliaji pale ambapo jengo linakuwa limejengwa chini ya viwango vya ubora na hivyo kuwa ngumu kufuatilia hata pale jengo linapodondoka kwakuwa hakuna utaratibu uliowekwa kisheria kwaajili ya kuwadhibiti wataalamu wa ujenzi pale wanapojenga majengo yaliyo chini ya viwango.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa bodi ya usajili ya wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi (AQRB) msanifu wa majengo Ambwene Mwakyusa alipokutana na wadau wa ubunifu majengo na wakadiriaji majenzi, jijini Dar es salaam

Kwa upande wake msajili wa bodi ya wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi, msanifu wa majengo Jehad Jehad, amesema kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu kuwepo kwa vifaa duni katika sekta hiyo, jambo ambalo imebidi bodi hiyo kumuita mtu wa shirika la viwango la taifa (TBS) kwaajili ya kuwahakikishia wataalamu hao jitihada zinazofanyika kudhibiti hali hiyo.

Bodi ya usajili ya wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi AQRB pia imewataka wadau wake kuhakikisha kwa mujibu wa sheria inayowaongoza namba 4 ya mwaka 2010 kuwa na bima ambayo itamkinga mtaalamu kwa makosa atakayofanya

No comments:

Post a Comment