Thursday 12 May 2016

Serikali kunufaika na zaidi ya bilioni 24 kupitia bahati nasibu


Serikali ya Tanzania itarajie kupata mapato ya shilingi bilioni 24 yatakayokusanywa kama kodi kutokanana bahati nasibu ya taifa itakayoanza hivi karibuni.
Kuanza kwa Bahati Nasibu hiyo kunatokana na kuanza kwa mkataba wa kibiashara chini ya uwekezaji wa pamoja baina ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini na mwekezaji Kampuni ya Murhandziwa kutoka nchini Afrika Kusini. 

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Bw. Abbas Tarimba, amesema hayo leo na kwamba mbali ya mapato hayo, zaidi ya ajira elfu kumi za moja kwa moja zitapatikana baada ya wawekezaji hao wawili kurejesha upya Bahati Nasibu ya Taifa inayotarajia kuanza Mei 21 mwaka huu.

"Bahati Nasibu hii ina umuhimu mkubwa kwa uchumi wa nchi, kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao tunategemea kuipatia serikali takribani shilingi bilioni 24 kama kodi kutokana na biashara tutakayoifanya," amesema Bw. Tarimba.

Ameongeza kuwa hata mchango wa sekta ya michezo ya kubahatishja kwenye uchumi nao utaongezeka kwani hivi sasa sekta hiyo inachangia asilimia 1.5 ya pato la taifa.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampuni ya Murhandziwa Profesa Bongani Khumalo amesema hatua ya kuja kuwekeza nchini imetokana na kuridhishwa na jinsi serikali inavyosimamia utendaji wa bodi ya michezo ya kubahatisha kiasi cha kuifanya kuwa moja ya bodi zenye heshima kubwa barani Afrika.

No comments:

Post a Comment