Azam FC chini ya Kocha Aristica Cioaba raia wa Romania haijafurahishwa na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Yanga, hivyo wamesema leo watamaliza hasira zao kwa kuifunga Ndanda FC.
Wikiendi iliyopita, ikicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam, Azam ilipoteza mechi yake ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga.
Cioaba alisema watapambana kuhakikisha wanashinda mechi ya leo dhidi ya Ndanda kwenye uwanja wao wa nyumbani ili waisogelee Simba kileleni.
Simba ipo kileleni mwa ligi ikiwa na pointi 35 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 30. Yanga ni ya tatu ikiwa na pointi 28.
“Timu nzima iko vizuri isipokuwa tutamkosa Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ ambaye ana kadi nyekundu, wachezaji wengine wapo tayari kwa ajili ya mechi hii hata beki wetu Daniel Amoah naye atakuwepo.
“Tunataka kushinda mechi hii ili tuwasogelee waliotupita na naamini tutafanya vizuri na kurudi katika mbio za ubingwa,” alisema Cioaba. Mechi ya Azam na Ndanda itachezwa saa 1:00 usiku.
No comments:
Post a Comment