Friday 13 May 2016

LHRC yaonya vitendo hivi kwa Jamii kuhusu wahanga


  Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) Dkt. Hellen Kijo-Bisimba amekemea na kuitaka jamii kuacha kabisa kuwavunjia haki zao za kimsingi kwa makusudi wahanga wa matukio mbalimbali ya ajali na vitendo vya kiukatili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) Dkt. Hellen Kijo-Bisimba amekemea na kuitaka jamii kuacha kabisa kuwavunjia haki zao za kimsingi kwa makusudi wahanga wa matukio mbalimbali ya ajali na vitendo vya kiukatili kwa kutuma na kusambaza picha za wahanga hao zikionyesha majeraha au hata maiti za watu hao kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kinyume cha tarataibu na haki za binadamu zinavyoelekeza.

Dkt. Kijo-Bisimba ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akitoa tamko la pamoja linalojumuisha mashirika yanayofanya kazi za utetezi wa haki za binadamu hasa zile zinazohusu makundi maalum na kuongeza kuwa ni wajibu sasa kwa kila Mtanzania kwa kushirikiana na serikali pamoja na mashirika mbalimbali kukemea na kuwafichua watu wanaojihusisha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Ameiasa jamii ya watanzania kuacha ushabiki badala yake tutumie mitandao hiyo ya kijamii katika kuelimisha na kujadili masuala mbalimbali ya maisha ambayo yanalinda na kuheshimu haki za binadamu pamoja na shighuli zingine za kimaendeleo na zenye kuleta tija kwa taifa na kwa mtu mmoja mmoja na kuiomba serikali kwa kushirikiana na mamalaka ya mawasiliano nchini TCRA kuchukua hatua kali za kisheria na mahususi bila kujali vyeo vya watuhumiwa wa makosa hayo kwenye jamii.

Kuhusu Sheria ya Mitandao iliyopitishwa na Serikali, Dkt. Kijo-Bisimba amesema sheria hiyo inaonekana imekuja kwa ajili ya kuilinda serikali na sio kulinda mtu mmoja mmoja kama ilivyotegemewa na Watanzania wengi.

No comments:

Post a Comment