MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa siku 90 kwa viwanda vinavyozalisha mifuko ya plastiki, kutozalisha mifuko hiyo kwa kuwa imekuwa ikichangia katika uchafuzi wa mazingira.
Pia amewataka wazalishaji wa mifuko hiyo, kuiga mfano wa Zanzibar, ambayo imefanikiwa kudhibiti matumizi ya mifuko hiyo.
Alitoa agizo hilo jana wakati akizindua kampeni ya usafi ya siku 90 yenye lengo la kuhakikisha mkoa huo unakuwa na mazingira safi ambayo itahusisha mashindano ya mitaa ya jiji, iliyopangwa na isiyopangwa.
Hatua hiyo imefikiwa kutokana na agizo la Rais John Magufuli alilotoa Desemba mwaka 2015, ambapo katika utekelezaji wake, Makonda amebuni shindano hilo ambalo mshindi atapata Sh milioni 50.
“Naomba muige watu wa Zanzibar, wana mifuko lakini si ya plastiki. Ndani ya siku 90 kuanzia leo (jana) sitaki kuona mifuko ya plastiki ndani ya mkoa wangu... Tuachane na hii mifuko ambayo kwanza kimsingi ni ngumu kuiteketeza, lakini hata ukiamua kuiteketeza madhara yake ni makubwa,” alisema Makonda.
Katika hatua nyingine, Makonda amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Theresia Mmbando, kuanzia kesho aunde kamati ya uchunguzi wa kampuni za usafi zinazomilikiwa na watumishi wa umma, ili ziondolewe kwa kuwa ni kinyume cha maadili ya utumishi wa umma.
Alisema katika mkoa huo kuna watumishi wameanzisha kampuni za kusafisha miji, lakini kwa mujibu wa maadili ya utumishi wa umma kipengele cha mgongano wa maslahi hakiruhusu watumishi kumiliki kampuni za kutoa huduma hizo kwa jamii.
“Pia naagiza waende kuangalia, kampuni nyingi zinazopewa zabuni hazina vifaa kama zilivyoeleza kwenye makaratasi yao, wamejieleza kuwa na magari saba, wafanyakazi 100 na mifagio lakini ukienda wanapofanya usafi hakuna kitu,” alisema.
Alisema mkoa huo hutumia zaidi ya Sh bilioni sita kwa mwaka kukusanya uchafu, lakini bado jiji linakuwa chafu na kutaka fedha hizo ziendane na matokeo ya usafi uliokusudiwa. Aidha aliwaasa vijana kufanya kazi ili kuleta maendeleo kwani Rais Magufuli anawaamini vijana na kuonesha kuwa wamelelewa vizuri na kufundishwa uadilifu na kupewa moyo wa kujituma na kufanya kazi.
“Usikubali kumuona mtu anachafua mazingira na wewe ukiwepo. Lakini matrafiki wote kuanzia Jumatatu (kesho), nataka mkague daladala kama wameweka chombo cha taka ndani ya magari yao,” alisema.
Pia aliwataka makondakta kuhamasisha watu kuwa wasafi kwa kuelekeza abiria sehemu ya kutupa taka wawapo ndani ya daladala. Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, kutoa taarifa za hatua alizowachukulia maofisa watatu wa wilaya hiyo walioshindwa kutekeleza majukumu yao katika kufanikisha kampeni hiyo.
“Ifikapo Jumanne mchana, niwe nimepata taarifa za hatua za kinidhamu walizochukuliwa watumishi hawa ambao ni Abiyu Peter, Ofisa Usafishaji, Ofisa Utumishi, Josia Kiverenge na Ofisa Utamaduni, Joyce Kirio,” alisema.
No comments:
Post a Comment