MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amesema kuwa Bohari ya Dawa (MSD) ni jipu, linalohitaji kutumbuliwa kwa kuwa haiwezekani taasisi ya serikali kuwa kigango cha udalali kwa watu wachache kujitengenezea fedha.
Hapi alisema wataandika barua kwa Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda kwenda kwa Rais John Magufuli atumbue jipu hilo kwani MSD wananunua dawa katika maduka ambayo watumishi wa afya wana uwezo wa kununua kwa bei nafuu.
Kauli hiyo ameitoa baada ya Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Aziz Msuya kutoa malalamiko hayo mbele yake kwenye mkutano wa watumishi wa afya uliofanyika Kinondoni, Dar es Salaam.
Dk Msuya alisema kuwa watumishi wa afya wanatukanwa na kuchukiwa na wananchi kutokana na uhaba wa dawa na kwamba wanapoagiza dawa MSD, wanapewa kidogo kuliko hundi wanazoziandika.
‘’Tunafuata utaratibu wa serikali, kwa mfano tunaweza kuandika hundi ya Sh milioni tano kwenda MSD kununua dawa lakini jambo la kushangaza, tunaletewa dawa chache zisizolingana na fedha tuliyotoa na pia hawaturudishii fedha iliyobaki wala kutuambia kama hakuna dawa nyingine, ’’ alisema Dk Msuya.
Pia alisema kuwa MSD wananunua dawa katika maduka ya Salama yaliyopo Kariakoo na kudai wakiachiwa watumishi hao wanaweza kununua wenyewe kwa bei nafuu kuliko wanazotozwa na MSD.
Akitoa mfano, Dk Msuya alisema kopo moja la dawa ya Panadol huuzwa Sh 7,000 wakati MSD inauza Sh 14,000 hivyo wameona kuwa bei hiyo ni ghali kuliko wakienda kununua wenyewe madukani.
Aliongeza kuwa ikiwezekana MSD isiwazuie kwenda kununua dawa na vifaa tiba katika maduka ambayo wana uhakika wataweza kupata vitu vyote wanavyohitaji kuliko wao kuwaletea vitu nusu nusu ambavyo wakati mwingine sio mahitaji ya haraka ya hospitali husika.
Kutokana na malalamiko hayo, Hapi alisema kuwa inapaswa kujulikana fedha zinazobaki MSD baada ya kupeleka dawa chache katika hospitali zinafanyiwa nini na kama kuna uwezekano wa kununua dawa wenyewe kuondoa usumbufu uliopo.
‘’Pia naagiza kuandikwe barua kwenda Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (Temesa) kuulizia gharama za kugagua uwekaji wa jenereta katika Hospitali ya Sinza Palestina unafuata utaratibu gani kwa maandishi kwani haiwezekani wanataka malipo ya ukaguzi wa kabla na baada ya kuweka jenereta hilo,’’ alisema Hapi.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa suala la mashuka katika Hospitali ya Mwananyama ni tatizo na kuagiza mtunza stoo kujieleza kwa nini asichukuliwe hatua baada ya kubainika kuficha mashuka 20 huku wagonjwa wakilalia vitanda bila mashuka.
Pia aliagiza kusitishwa kwa mkataba na mzabuni ambaye ni Yunik anayefua mashuka hayo kutokana na kuchanika kwa mashuka mengi na kuwa mepesi kutokana na matumizi ya dawa kali za kufulia.
Hadi Mei 18 mwaka huu mtaniambia mapendekezo yenu kuhusiana na suala hili,’’ alisema Hapi.
Aidha, akijibu hoja hiyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk Delila Moshi alisema kuwa mwaka huu wameagiza mashuka 250 na MSD inawauzia shuka moja kwa Sh 16,700 huku kitanda kimoja kikihitaji mashuka nane. Dk Moshi alisema wana vitanda 250 na mashuka 350 hivyo mashuka yote yakifuliwa, kunakuwa na upungufu siku inayofuata.
No comments:
Post a Comment