Monday, 9 May 2016

Rais Dk.Magufuli:Mimi sio jeuri wala katili

 
RAIS John Magufuli amesema hatua anazochukua dhidi ya watumishi wa umma waliofanya ubadhirifu serikalini na taasisi zake zinalenga kuwarudisha kwenye maadili ya utumishi wa umma, kufuata misingi ya kazi na sio vinginevyo.

Alisema hayo jana katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Burka mjini hapa alikoshiriki ibada na waumini wa kanisa hilo. Rais Magufuli alisema watumishi wa umma walijisahau, wakafanya ubadhirifu na kukiuka kwa makusudi maadili ya kazi kwa hali ya juu na kufanya Watanzania wanyonge kuendelea kuteseka wakati wao wakiendelea kuishi maisha ya peponi.

Alisema anapambana na watumishi hao kwa hali na mali na atawasimamisha kazi na hata kuwafukuza kazi kwa kuwa aliahidi kutetea wanyonge. Alisisitiza hilo kwake halitarudi nyuma. Rais alisema yeye sio mkatili wala jeuri kama ambavyo baadhi ya watu wanafikiria.

Alisema kwa hali ilivyokuwa, ni lazima achukue hatua madhubuti kwa watumishi wa umma walioifilisi nchi kwa manufaa yao, iweze kusonga mbele. ‘’Mimi sio mkatili wala jeuri, lakini ni lazima uchukue hatua kwa watumishi wa umma walioifikisha nchi hapa tulipo,’’ alisema.

Aliongeza kusema; “Nimejitoa kafara kwa ajili ya wanyonge kama nilivyoahidi kipindi nilipokuwa naomba kura kutaka niwe Rais na hilo litawaudhi baadhi ya watu wakubwa, lakini itabidi wanivumilie tu.

“Niko pamoja na ninyi ndugu zangu Watanzania na wana Arusha wote, napenda kuwaahidi tena sitawaangusha, nitasimama mbele kuwatetea masikini. Siku zote nitakuwa upande wenu, siku zote nitatembea na ninyi, nasema kwa dhati kabisa na nataka muamini hilo kwamba sitawaangusha,” alisema Magufuli huku akishangiliwa na waumini walioshiriki ibada hiyo.

Rais ambaye alisisitiza kukerwa na hali mbaya ya kimaisha ya Watanzania wanyonge wakati baadhi ya watumishi wa umma wakiishi kama wako peponi, alisema kasi yake ya kupambana na watumishi hao hataipungua kamwe na ndiyo kwanza inaanza.

“Najua baadhi ya wakubwa watakerwa na hatua ninazochukua, kwa hiyo nawaomba Watanzania mniombee kwa Mungu ili niweze kufanya kazi yangu kwa amani kubwa, ‘’Watumishi wamejisahau na wamekuwa wakifanya kazi kinyume na maadili ya utumishi wa umma na hatua ninazochukua msizitafsiri kuwa ni ukatilii au udikteta hapana,’’ alisema.

Rais Magufuli alisema, ‘’Watumishi wa umma wamekuwa wakiwadhulumu Watanzania kwa muda mrefu kwa kuwanyonya jasho lao; hivyo ni lazima maamuzi ya kuwarudisha katika mstari yachukuliwe.”

Alisema ili nchi iweze kupiga hatua lazima kuwe na nidhamu ya kazi, uadilifu na kuwajibishana linapokutwa kosa. Alisema bila ya hivyo, nchi haiwezi kusonga mbele itakuwa ni kujidanganya. Rais aliongeza kuwa Watanzania wanyonge ni lazima wapate haki yao pale wanapohitaji na kutokuwa na matabaka ya walionacho na wasio nacho.

“Ninajua kuongoza ni kazi kubwa, ninajua kuongoza taifa lililo masikini kama Tanzania inahitaji mkono wa Mungu, kwa hiyo niwaombe sana ndugu zangu Wakristo na Watanzania kwa ujumla, muendelee kuliombea taifa hili, kuniombea mimi, na pia kujiombea sisi wote ili amani tuliyonayo katika nchi yetu iendelee kudumu katika maisha yote.

“Lakini siku zote katika matendo yetu kila tunapofanya tumtangulize Mungu kwa sababu Mungu ndio kila kitu, lakini tutambue kwamba siku moja tutakufa, kwa hiyo ni vyema katika matendo yetu tutakapokuwa hapa duniani tujitahidi sana kufanya matendo mazuri kwa ajili ya watu na hasa watu wanyonge, ambao kwa kweli Watanzania waliowanyonge wanapata shida sana,” alisema.

Akihubiri kwenye ibada ya misa takatifu kanisani hapo, Padri Geramani Longoi, aliwataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii na kuwa waadilifu kazini. Katika misa hiyo ya Siku Kuu ya Kupaa Mbinguni kwa Yesu Kristo, Longoi alisema hata Yesu Kristo alifanya kazi yake duniani na baada ya kuwatumikia ipasavyo wanadamu, alipaa mbinguni.

Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Jonathan Mushi aliwataka Watanzania kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi ngumu anayofanya. Mushi alisema kila Mtanzania mwenye nia njema na nchi yake, hanabudi kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kuwa uamuzi anaouchukua ni mgumu. Alisema uamuzi wake unataka kila mmoja kufuata maadili ya kazi na kuwa muadilifu.

No comments:

Post a Comment