Monday 2 May 2016

Rais Magufuli atua mzigo wafanyakazi

 Maguuuuuuuuuuu
RAIS John Magufuli ametangaza kushusha Kodi ya Mshahara (PAYE) kwa wafanyakazi hadi kufikia asilimia tisa kutoka 11 ya sasa kuanzia mwaka wa fedha ujao wa 2016/2017.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana mjini Dodoma wakati akihutubia Taifa katika Siku ya Wafanyakazi Duniani Kitaifa kwenye Uwanja wa Jamhuri na kusema amefanya hivyo ili kuwapunguzia mzigo wa kodi watumishi.

“Napenda kuwataarifu kuwa serikali yangu kama nilivyoahidi wakati wa kampeni zangu, nimeamua kupunguza kodi ya mapato ya mishahara kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia tisa kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/2017, nikiwa na matarajio makubwa kuwa wabunge wataipitisha Bajeti yangu niliyoiwasilisha bungeni,” alisema Rais Magufuli na kushangiliwa na maelfu ya wafanyakazi waliofurika uwanjani hapo.

Awali, katika risala yao, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholaus Mgaya alisema licha ya kwamba wafanyakazi wamekuwa na kilio cha muda mrefu cha kulipwa Kima cha Chini cha Mshahara kisichotosheleza kumudu kupanda kwa gharama za maisha, mshahara huo mdogo umekuwa pia ukitozwa kodi ambayo alieleza kuwa imekuwa ni ya mazoea kwa serikali kwa sababu ni rahisi kuikusanya.

“Tuna imani mzigo huu tuliokuwa tumebebeshwa wafanyakazi wa kulipa kodi kubwa ya mshahara utapungua. Aidha, tunaamini serikali haitoshindwa kupunguza Kodi ya Mishahara kuwa tarakimu moja. “Tunashauri Ofisi ya Msajili wa Hazina ipewe nafasi kubwa katika kusimamia ipasavyo mashirika ya umma ili kuongeza na kuchangia Pato la Taifa. Aidha, tunapendekeza kodi inayokatwa kwenye malipo yatokanayo na Mikataba ya Hali Bora Kazini iangaliwe upya,” aliongeza Katibu Mkuu wa Tucta.

Magufuli alisema kwa kufanya hivyo atakuwa amewapunguzia wafanyakazi mzigo mkubwa wa makato katika mishahara yao na ameamua kuanza na jambo hilo kwanza ili changamoto zilizopo za kiuchumi wazikabili.

“Tutaangalia lakini tutakaa na viongozi wenu wa Tucta ndani ya serikali tuangalie kadiri uchumi utakavyokuwa unaenda tuangalie ni namna gani tutaweza kuongeza mishahara ya watumishi wetu,” alisema Dk Magufuli.
Aidha, alisema kwa sasa ameamua kushusha kwanza kodi hiyo ambayo imekuwa ni mzigo mkubwa kwa wafanyakazi wengi na baadaye mambo yakiwa mazuri wataangalia namna ya kupandisha mishahara.

Alisema kupunguza kiasi hicho cha asilimia mbili ni wazi kuwa kutakuwa na pengo kubwa la makusanyo ndani ya serikali na watalazimika kulifidia kwa njia nyingine huku kukiwa na kawaida ya watu pekee wasiokwepa kulipa kodi wakiwa ni wafanyakazi.
Alisema kwa sasa serikali itaangalia ni namna gani itaweza kufidia pengo hilo la gharama za kodi ambazo zilikuwa zikilipwa na wafanyakazi katika upande mwingine. 

Akizungumzia uwiano wa mishahara, alisema nchini wapo watu wanalipwa mishahara ya chini sana na wapo wanaolipwa mishahara ya juu sana huku kazi zikifanywa na watu wa chini na wao wakipata mishahara mikubwa.
Alisema alikwishakuzungumzia suala hilo hadharani na analirudia tena kuwa mwisho itakuwa ni Sh milioni 15 ili hizo nyingine zipelekwe kwa watumishi wengine waliokuwa wakipata mishahara midogo.

“Nilikwishazungumza hadharani na leo narudia, wale waliokuwa wanapata mishahara mikubwa, nimeshasema itakuwa mwisho ni milioni 15 kushuka chini ili hizi zingine tuzi ‘save’ tuwapelekee watumishi waliokuwa wakipata mishahara midogo,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema wasiotaka kufanya kazi kwa kuwa walikuwa wakipata mishahara mikubwa, waache kazi mara moja kwani haiwezekani katika nchi moja mtu mwingine anapata mshahara wa Sh milioni 30 huku mwingine anapata mshahara wa Sh 300,000.

Alisema serikali katika kutafuta uwiano sawa katika mishahara, ameunda bodi mbili za mishahara ya watumishi wa sekta binafsi na utumishi wa umma na majukumu ya bodi hizo ni kufanya uchunguzi na kupendekeza kima cha chini cha mshahara na anaamini kuwa bodi hizo zilizoundwa kutokana na marekebisho ya Sheria ya Kazi Namba 4 ya mwaka 2004 zinafanya kazi zake ilivyokusudiwa.

Akijibu hoja ya serikali kuhamia Dodoma, Rais Magufuli alisema tayari yeye kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wameshahamia Dodoma na hata yeye huenda Dodoma na kukaa Ikulu ya Chamwino.

“Zile hoja nyingi ambazo zimetolewa na Katibu Mgaya, wa Tucta hasa zile za kuhamia Dodoma… nikaanza kumuuliza rais wake hivi makao makuu ya Tucta yako wapi? Akasema yapo Mnazi Mmoja Dar es Salaam. Kwa hiyo nikamuuliza wewe Mukoba unakaa Dar es Salaam Mnazi Mmoja? Ndiyo, na Mgaya makao makuu yake yapo Dar es Salaam? Ndiyo.

Kwa hiyo pamoja na hoja ambazo amezitoa hapa akiomba serikali yangu ihamie Dodoma yeye hajaanza mfano wa kuhamia Dodoma…Kazi hizi ndugu zangu ni ngumu,” alisema Magufuli.
Alikipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuonesha mfano wa kuhamia Dodoma na kutaka vyama vingine viunge mkono kwa kuhamia katika mji huo mkuu wa Tanzania.

Alisisitiza nia ya serikali kuhamia Dodoma iko pale pale hasa kwa kuwa suala hilo limeelezwa bayana katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Alisema ni vyema wale wote ambao wanataka serikali kuhamia Dodoma wakaonesha mfano kwa vitendo ili serikali nayo sasa iige mfano huo na kuhamia Dodoma.

Hifadhi ya jamii Rais Magufuli katika hotuba yake hiyo, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imelenga katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafaidika na mfumo wa hifadhi ya jamii nchini kuliko ilivyo sasa kwa kuona wananchi wengi zaidi wanajiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili wawe na uhakika wa matibabu.
Alisema serikali inaendelea na juhudi za kupanua wigo wa huduma za Mfuko wa Afya Jamii (CHF) na pia kuwawezesha wafanyakazi wengi wa sekta binafsi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Aidha, alisema mifuko ya hifadhi ya jamii imeanza kusajili wanachama kutoka sekta zisizo rasmi ikiwa ni lengo la serikali kuona wananchi wengi wanapata huduma za msingi za hifadhi ya jamii.

Alisema pia wameitaka mifuko ya hifadhi ya jamii kuachana na uwekezaji usio na tija na badala yake kuangalia uwekezaji wenye manufaa kama kuanzisha viwanda ambavyo vitaajiri watu wengi na wao kupata wanachama.

Rais alisema ombi la Tucta juu ya kupunguza mifuko ya hifadhi ya jamii na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima wamelipokea na kuahidi kulifanyia kazi katika kipindi cha mwaka wa fedha ujao 2016/2017 unaoanza Julai mosi.

Na Habari Leo

No comments:

Post a Comment