Thursday, 4 August 2016

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA Harry Kitilya na Wenzake wafungua kesi ya kikatiba yakupinga Kunyimwa Dhamana.


Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha katika kesi mbili tofauti wamefungua kesi ya kikatiba wakipinga kunyimwa dhamana. 

Kitilya, Shose Sinare na Sioi Solomon, wanaoshtakiwa katika kesi moja na nyingine ya utakatishaji fedha inayomjumuisha, Gidion Wasongo wamefungua kesi hiyo Mahakama Kuu. 

Mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wa pili ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkurugenzi wa Mashtaka ( DPP). 

Kesi hiyo ya kikatiba namba 14 ya mwaka 2016, Kitilya na wenzake wanapinga kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinachozuia dhamana kwa mashtaka ya utakatishaji fedha.

Wanadai kuwa kifungu hicho kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya mwaka 1977, Ibara ya 13 (b).

Ibara hiyo inazuia mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo. 

Pia, wanadai uamuzi wa kuwafungulia shtaka la utakatishaji fedha haukuwa wa haki, bali ulikuwa na nia mbaya ya kuwanyima dhamana.

Kesi hiyo imepangwa kuanza kutajwa leo mahakamani hapo, kabla ya kuendelea na taratibu nyingine za usikilizwaji wa hoja za  msingi za wadai hao. 

Wakati Kitilya, Sinare na Sioi wakikabiliwa na shtaka hilo katika kesi moja, Wasongo anakabiliwa na shtaka hilo katika kesi tofauti yeye na wenzake wengine akiwamo aliyekuwa Mhasibu wa TRA, Justice Katiti. 

Hata hivyo, licha ya kesi hiyo ya kikatiba, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga kutoa uamuzi wa rufaa dhidi yao Agosti 9, ambayo DPP anapinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kuwafutia shtaka la utakatishaji fedha. 

Katika kesi ya msingi, Kitilya na wenzake wanakabiliwa na mashtaka manne ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kujipatia fedha Dola za Marekani 6 milioni kwa njia za udanganyifu na kutakatisha fedha kiasi hicho, ambalo liliwafanya wakose dhamana. 

Hata hivyo, ilikuwa ni furaha kwao baada ya Mahakama hiyo baadaye kuwafutia shtaka hilo, kutokana na juhudi za mawakili wao, Dk Ringo Tenga, Majura Magafu na Alex Mgongolwa kulipinga kuwa halijakidhi vigezo vya kisheria kuitwa kosa la utakatishaji fedha. 

Lakini DPP hakukubaliana na uamuzi huo wa Mahakama ya Kisutu, hivyo alikata rufaa Mahakama Kuu, lakini Mahakama Kuu katika uamuzi uliotolewa na Jaji Moses Mzuna ilitupilia mbali rufaa hiyo pamoja na mambo mengine akieleza kuwa hapakuwa na haja kukata rufaa kwa uamuzi huo. 

DPP hakukubaliana pia na uamuzi huo wa Mahakama Kuu, hivyo alikata rufaa Mahakama ya Rufani na akashinda na mahakama hiyo iliamuru Mahakama Kuu isikilize upya rufaa ya DPP.


USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment