Thursday 4 August 2016

Hivi ndivyo Tundu Lissu alivyokamatwa na Jeshi la Polisi Akiwa Singida.

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amekamatwa na polisi muda mfupi baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Ikungi, Singida. 

Wakati Lissu akiwa mikononi mwa polisi, Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa jana alifanya mkutano wa hadhara na kusema hakuna wa kumpangia cha kuzungumza kwenye mikutano yake. 

Kukamatwa kwa Lissu 

Lissu, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema ndiye aliyetoa taarifa za kukamatwa kwake kwenye mtandao akisema: “Wakubwa sana salaam. Ninawaandikieni maneno haya nikiwa chini ya ulinzi wa polisi Singida.

" Nimemaliza kuhutubia mkutano wa hadhara mji mdogo wa Ikungi ambao ni makao makuu ya Jimbo langu la Singida Mashariki. Mara baada ya kushuka jukwaani nimefuatwa Regional Crimes Officer (RCO) wa Mkoa wa Singida aliyejitambulisha kwa jina la Babu Mollel na kunitaarifu kuwa ameelekezwa na Regional Police Commander (RPC) Singida nikamatwe apparently (dhahiri) kuna amri ya kunikamata iliyotoka Dar es Salaam.

 “Kwa hiyo niko nguvuni na ninasubiri maelekezo ya RPC juu ya wanakotakiwa kunipeleka. It’s likely (inawezekana) nitasafirishwa Dar usiku huu. In fact (hakika) ni usiku huu kwa taarifa za sasa hivi. Kwa vyovyote itakavyokuwa, there’s no turning back. There’s no shutting up (hakuna kurudi nyuma, hakuna kunyamaza). 

"Nitapambana kutetea haki yetu ya kuwasema watawala popote nitakapokuwa, whether in freedom or in jail (niwe huru au jela)... Aluta continua!. "

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka  alithibitisha kukamatwa kwa Lissu lakini alikataa kutoa sababu za hatua hiyo. 

Chadema jana jioni ilitoa taarifa kuhusiana na kukamatwa kwa Lissu ikisema: “Tunaweza kuthibitisha kwa vyombo vya habari kuwa Mwanasheria Mkuu wa Chama Mh. Tundu Lissu anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Singida kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi.” 

Taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene ilibainisha kuwa Polisi walimkamata jana jioni baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara alioufanya Ikungi jimboni kwake na kueleza kuwa viongozi wa chama hicho mkoani humo walikuwa polisi kuhakikisha anapata haki zake kama inavyostahili na kwamba ofisi ya katibu mkuu inafuatilia kwa ukaribu kujua sababu hasa ya kushikiliwa kwake na kutoa msaada wa haraka kadri itakavyohitajika. 

Lissu amekuwa kwenye misukosuko na Jeshi la Polisi mara kadhaa na kwa siku za karibuni alikamatwa na kufikishwa mahakamani akituhumiwa kutoa maneno ya uchochezi kwenye gazeti la Mawio. 

Sambamba na kesi hiyo, Lissu alikamatwa na polisi kwa madai ya kutoa maneno ya uchochezi baada ya kupata dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. 


No comments:

Post a Comment