Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge kwa niaba ya wenzake Mbunge wa Kawe Halima Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) amesema
 
wamekasirishwa na kitendo cha Mbunge wa Ulanga kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Goodluck Mlinga.

''Wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Katiba na Sheria Mbunge Mlinga alisema kwamba wabunge wa UKAWA hususani Chadema ili waweze kuwa wabunge wa viti maalum ni lazima wawe na mahusino ya kimapenzi na viongozi wao ili waweze kuchaguliwa jambo hilo limetudhalilisha kwa sababu sisi huwa tuna utaratibu wa chama wa kikatiba ambao huwezesha mbunge kuchaguliwa kutokana na uwezo wake wa kisiasa ili aweze kuja kulitumikia taifa''- Amesema Halima Mdee.

Mdee ameongeza kuwa kufuatia kauli hiyo wameomba muongozo kupitia kwa Mbunge wa viti maalum Sophia Mwakagenda ambapo Naibu Spika alimtaka Mbunge huyo kuomba radhi jambo ambalo halikufanikiwa. 

Aidha wabunge hao wameongeza kuwa kutokana na kudhalilishwa huko huku Naibu Spika ambaye pia ni mwanamke akiacha jambo hilo libakie hivyo na wakati huo huo wabunge wanawake wanaounda umoja wa wabunge wakishangilia ni dhahiri wamedhalilishwa hivyo wabunge wanawake wa UKAWA 
wametangaza kujiondoa kwenye umoja wa wabunge wanawake na kuwaacha wanawake wabunge wa CCM pekee.