WAKATI abiria wa mabasi yaendayo haraka wanaanza kulipa nauli leo na kuingia katika vyombo vya usafiri kwa foleni, imebainika kuwa mfumo wa uchanjaji kadi haujakamilika, hali itakayowalazimu abiria kutumia tiketi za kawaida.
Mfumo wa kuchanja kadi unamwezesha mtumiaji kuweka tiketi au kadi katika eneo maalumu la mashine ya utambuzi, ambapo inatambuliwa na kumwezesha abiria kuingia katika kituo cha daladala kusubiri usafiri ama kutoka.
Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo ameziagiza mamlaka zote zinazohusika na mfumo huo wa kuchanja kadi kukamilisha haraka ili zianze kutumika.
Mamlaka zinazohusika na mfumo wa kuchanja kadi ni Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), Kitengo cha Serikali Mtandao, Benki Kuu (BoT) na Wakala wa huduma za mtandao (MaxMalipo).
Akitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam, Jaffo alisema ni vema mamlaka hizo zikahakikisha zinakamilisha mfumo huo haraka kuondoa ujanja wa watu kusafiri bila kulipa nauli.
“ Nawataka wakamilishe mfumo huu mara moja, kwanza itaondoa matumizi ya karatasi ambazo zinachafua mazingira, lakini pia utafanya baadhi ya watu kusafiri bila kukata tiketi alisema,” alisema Jaffo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya UDA-RT, David Mgwasa alisema kwa sasa abiria watalazimika kukata tiketi zenye alama maalumu zitakazotumika mpaka hapo mfumo wa kuchanja tiketi utakapokamilika, ambayo ni zaidi ya siku tano zijazo.
“ Kadi tunazo, lakini hatuwezi kuanza kuuza kwa sasa mpaka hapo mfumo wa kuchanja kadi utakapokamilika,” alisema. UDA-RT imeanza kutoa huduma ya mabasi ya haraka siku saba zilizopita na kwa siku sita mfululizo ilitoa huduma hiyo bure kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya huduma hiyo.
Aidha, Jaffo alitaka vyombo vya usalama kutofumbia macho wananchi wanaotumia miundombinu ya mabasi yaendayo haraka kufanya uhalifu na kutaka kuudhibiti katika vituo vya mabasi hayo.
Onyo hilo limetokana na ombi la Joseph Kinyamagoha, mkazi wa Kimara aliyetaka kuwepo ulinzi kutokana na watu wengi kuibiwa wakati wa majaribio ya utoaji wa huduma hiyo. “ Yeyote atakayekutwa anafanya uhalifu katika vituo hatafumbiwa macho, tutawakamata na tusije kulaumiana, onyo hili pia linakwenda kwa wananchi wenye vyombo vya moto ambao wanatumia miundombinu hii, hatutawafumbia macho,” alisema Jaffo.
Aliwataka UDA-RT kuhakikisha wanaweka mfumo utakaohakikisha wananchi wanapanga foleni wakati wa kuingia kwenye mabasi, jambo ambalo pia litapunguza tabia ya udokozi kwenye mabasi hayo.
Pia, aliitaka DART kutumia changamoto zilizojitokeza katika awamu ya kwanza ya mradi huo kama somo pindi wanapotekeleza awamu ya pili ambayo ujenzi wake unatarajia kuanza muda wowote mwaka huu na pamoja na awamu ya tatu.
Katika hatua nyingine, Mgwasa alisema leo huduma hiyo itaanza saa 11:00 alfajiri hadi saa sita usiku na mabasi 105 yatatatoa huduma katika njia kuu nne.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Peter Sima alisema jeshi limejipanga kuimarisha ulinzi katika miundombinu ya mabasi yaendayo haraka huku akiwataka wananchi kutumia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuvuka.
“ Watembea kwa miguu wanatakiwa kutumia alama zilizowekwa kwa ajili ya kuvuka. Ni marufuku pikipiki kutumia maeneo hayo na hata mwenye baiskeli anatakiwa kushuka anapovuka, ukikamatwa unavunja sheria za barabarani hutafumbiwa macho,” alisema Sima.
Mabasi hayo yamegawanyika katika aina mbili; ya haraka (express) yatakayosimama katika vituo takribani sita na ya kawaida yatakayosimama kwenye kila kituo.
Mabasi hayo yatafanya safari kati ya Kivukoni na Ubungo, Kivukoni na Kimara Mwisho, Kivukoni na Morocco, pia yapo yatakayofanya safari kati ya Kariakoo na Ubungo, Kariakoo na Kimara Mwisho; kati ya Kariakoo na Morocco, Morocco na Kimara Mwisho na kati ya Mbezi Mwisho na Kimara Mwisho.
Nauli kwa huduma hiyo ni Sh 400 kwa njia ya pembezoni (Mbezi- Kimara Mwisho), Sh 650 kwa safari za njia kuu huku wale wa njia kuu na pembezoni (Mbezi-Kivukoni au Kariakoo) ikiwa Sh 800.
No comments:
Post a Comment