Saturday, 28 May 2016

Wakala wa majengo Tanzania watoa uamuzi huu juu ya wanaodaiwa.

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA), umewapa muda watumishi wa umma waliokopa nyumba za Serikali mpaka wiki ijayo, wawe wamelipa madeni yao tofauti na hapo, watafukuzwa katika nyumba hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Elius Mwakalinga, alisema tayari wametoa notisi kwa watumishi hao ambayo inakwisha wiki ijayo, hivyo ni vyema watumishi hao wakalipa madeni yao kabla ili kuondoa usumbufu wanaoweza kuupata wakati watakapofukuzwa katika nyumba hizo.

“Tumeshafanya juhudi sana kwa wadeni wetu walipe madeni yao, lakini tunaona wengine bado hawajalipa na hatuna muda wa kuendelea kuwasubiri, kama wameshindwa tutawatoa katika nyumba hizo,” alisema Mwakalinga.

Aidha alisema kutokana na changamoto ya vifaa vya ujenzi visivyo na ubora kuingia kwenye soko la sekta ya ujenzi, Wakala huo umenunua vifaa vya kupima ubora wa majengo bila kuyaharibu.

Alisema vifaa hivyo ambavyo vina ubora wa hali ya juu vina uwezo wa kupima uimara wa zege lililokauka, kupima nondo na umbali uliowekwa pamoja na kupima muonekano wa ndani ya zege lililokauka. “Vifaa hivi vimeshawasili na kupokewa katika ofisi zetu na sasa mzabuni anatakiwa kuanza kutoa mafunzo jinsi ya kutumia vifaa hivyo,” alisema.

No comments:

Post a Comment