WAKATI katika majukwaa ya kisiasa ikielezwa kuwa viwanda vilivyokuwepo wakati wa ukoloni na vilivyojengwa muda mfupi baadaye, vimeuawa na kusababisha kukosekana kwa ajira, takwimu zinaonesha Tanzania ya sasa ni ya viwanda kuliko wakati wowote ndivyo vinavyoongoza katika kulipa kodi.
Akizungumza bungeni jana wakati akitoa hutuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17, kwa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Waziri wa wizara hiyo, Charles Mwijage, alisema mwaka 1961, Tanzania ilirithi viwanda 125 tu.
Waziri huyo mwenye jukumu la kutekeleza ahadi ya Rais John Magufuli, ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, aliweka wazi kuwa idadi hiyo ya viwanda vilivyorithiwa kutoka Serikali ya Kikoloni ni kidogo ikilinganishwa na viwanda vya sasa.
Mpaka mwaka 2005, wakati Serikali ya Awamu ya Nne ilipokuwa ikiingia madarakani, Mwijage alisema tayari viwanda vilikuwa vimeongezeka na kufikia 5,153.
Kwa mujibu wa takwimu hizo kuanzia mwaka 2005, kasi ya kuongezeka kwa viwanda nchini ilikuwa kubwa kuliko wakati wowote katika historia ya nchi, ambapo mpaka kufikia mwaka 2013, viwanda viliongezeka na kufikia 49,243.
Vilivyokufa
Akizungumzia viwanda vilivyokufa ambavyo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakivitumia kujenga hoja zao za kisiasa kuhusu ajira, Mwijage alisema viko 37 tu.
Alisema Serikali ilifanya tathmini katika viwanda vyote vilivyobinafsishwa ambavyo ni 106 na matokeo ya tathmini hiyo, yalibaini kuwa viwanda 45 vinafanya kazi vizuri; 24 vinasuasua na 37 tu ndio vimefungwa.
Ajira inayotolewa
Waziri Mwijage alisema kati ya viwanda hivyo 49,243, vikubwa ambavyo vimekuwa vikitoa ajira kuanzia watu 100 na kuendelea vipo 247.
“Viwanda vya kati vinaajiri kati ya watu 50 na 99 ni 170, viwanda vidogo vinavyoajiri kati ya watu watano na 49 ni 6,907 na viwanda vidogo sana vinavyoajiri chini ya watu watano ni 41,919,” alisema Mwijage.
Alisema ni lengo la Serikali ya Awamu ya Tano kuona viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinafanya kazi.
“Viongozi wakuu wa nchi wamekuwa wakisisitiza utekelezaji wa lengo hilo na wizara yetu kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina tunafuatilia jukumu hilo siku hadi siku,” alisema.
Kuongoza kodi
Wakati Mwijage akieleza hayo bungeni Dodoma, jijini Dar es Salaam, sekta hiyo ya viwanda imetajwa kuwa ndiyo inayoongoza katika ulipaji wa kodi za kampuni, ikifuatiwa na sekta ya benki huku taasisi za serikali zikiongoza katika ulipaji wa kodi za wafanyakazi.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari jana baada ya kuelezea makusanyo ya kodi ya Machi mwaka huu, Kamishna Idara ya Walipa Kodi Wakubwa wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Neema Mrema alisema viwanda ndio vinavyoongoza kulipa kodi.
Mrema alisema, kwa walipa kodi kuna kodi za aina mbili ambazo ni za kampuni na wafanyakazi ambapo kwa upande wa kampuni sekta inayoongoza ni ya viwanda ikifuatiwa na benki. “Lakini kwa upande wa kodi za wafanyakazi taasisi za Serikali ndio zinazoongoza katika kulipa kodi ikilinganishwa na zile za binafsi. Katika hili taasisi za serikali zinaongoza,” alisema Mrema.
Ufufuaji wa vilivyokufa
Kuhusu ufufuaji wa viwanda 37 vilivyokufa, Mwijage alisema mpango wa Serikali ni kuhakikisha viwanda hivyo vilivyofungwa baada ya kubinafsishwa, vinafanyiwa tathmini haraka kabla ya nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha unaoanza Julai Mosi, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mwijage, hatima ya viwanda visivyofanyakazi kwa sasa iko kwa wamiliki, ambao wamepewa kazi ya kutekeleza mikataba waliyoingia wakati walipouziwa na wakishindwa, viwanda hivyo wapewe wawekezaji wapya ili waviendeshe.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa kuhusu ubinafsishwaji, Serikali imeondokana na mzigo wa kutoa ruzuku ya kuendesha mashirika ya biashara yaliyokuwa chini yake.
Tanzania ya Magufuli
Mwijage alisema katika kuijenga Tanzania yenye uchumi wa viwanda, Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga kuhamasisha sekta binafsi ya Watanzania na wageni kuwekeza kwenye sekta ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.
Alisema katika kutimiza azma hiyo, Serikali itawekeza nguvu zaidi kwenye viwanda vidogo na vya kati (SMEs), kwa kuwa ndio kwa sasa vinavyoongoza nchini kwa kutengeneza ajira na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja.
Alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na wizara hiyo, sekta ya viwanda vidogo na vya kati imetengeneza ajira nyingi za Watanzania na kuchangia asilimia 28 kwenye Pato la Taifa (GDP).
Kwa mujibu wa Waziri Mwijage, pia wizara hiyo itawezesha upatikanaji wa maeneo ya kujenga viwanda na kutoa ushauri kuhusu upatikanaji wa mitaji na teknolojia za kisasa. “Kwa ujumla wizara itabeba jukumu la kuibua wana viwanda, kuwakuza na kuwaendeleza,” alisema.
Mazingira bora
Alifafanua kuwa kwa kuzingatia msimamo huo, wizara hiyo itahakikisha viwanda vilivyopo vinafanyakazi kwa uwezo mkubwa kadri iwezekanavyo, ili kudhibiti bidhaa za nje zinazoingia nchini bila ushindani ulio sawa.
Alisema pia wizara hiyo itaondoa vikwazo vinavyopunguza uwezo wa kiushindani kwa viwanda vilivyopo nchini, itahamasisha wananchi kuwekeza katika sekta ya viwanda na itahamasisha wawekezaji wakubwa wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta hiyo.
“Nawaahidi tutapigania kufa na kupona ili tuwe na miundombinu wezeshi na saidizi iliyo tayari katika maeneo ya uwekezaji ngazi ya Kanda na Taifa. “Nawashawishi wazawa wamiliki viwanda... huu ndio wakati. Tutalinda viwanda vyenu, siwezi kulisha mtoto wa kware na kuacha wa kuku afe,” alisema.
Alisema wizara hiyo itakuwa mboni kudhibiti taasisi za serikali ambazo utekelezaji wake unaiweka Tanzania katika nafasi mbaya kwenye kuvutia wawekezaji duniani.
Mwijage alisema mpango wa Serikali hiyo katika kutekeleza mkakati wa kujenga viwanda nchini, ni kuhimiza na kusimamia usambazaji wa viwanda sehemu zote za nchi na mamlaka za mikoa na wilaya zimeelekezwa kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli ya viwanda na biashara.
Maoni ya Kamati
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara, Vicky Kamata alipongeza hatua ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuleta mapinduzi ya viwanda, lakini alishauri hatua madhubuti zichukuliwe katika kushughulikia changamoto zinazoweza kukwamisha ndoto hiyo.
Aliitaka Serikali kuweka kipaumbele suala la kutenga ardhi kwa ajili ya viwanda kwa kushirikisha halmashauri za wilaya na mikoa, ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu bora kama vile barabara, reli, maji, umeme na mawasiliano.
Wakati akichangia bajeti hiyo, mbunge wa Msalala Ezekiel Maige (CCM), alishauri katika kutekeleza lengo la kujenga Tanzania ya viwanda, ni vyema Serikali iondoe changamoto zilizopo katika sekta ya uwekezaji.
Wizara hiyo imeomba kupitishiwa bajeti ya Sh bilioni 81.87, kati ya fedha hizo Sh bilioni 41 sawa na asilimia 51 ya bajeti ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh bilioni 40 sawa na asilimia 49 ya bajeti kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Imeandikwa na Halima Mlacha, Dodoma na Katuma Masamba, Dar
No comments:
Post a Comment