Saturday 4 June 2016

Haya ndio yakioandikwa katika Jarida maarufu la kila mwezi la Uingereza la Economist kuhusu Rais Dk.Magufuli.

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesema Rais John Magufuli amepaisha kasi ya uwekezaji nchini, ikielezwa ndani ya miezi sita ya utawala wake amevutia wawekezaji wapya 551.

Idadi hiyo ya wawekezaji katika miradi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 9,211.88 (karibu Sh trilioni 2), ni sawa na ongezeko la asilimia 20.

Miradi hiyo imeandikishwa kuanzia Desemba mwaka jana hadi Mei mwaka huu, ambapo kati ya miradi hiyo 229 sawa na asilimia 42 inamilikiwa na Watanzania na miradi 251 sawa na asilimia 39 inamilikiwa na wageni na miradi 107 inamilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na wageni.

Taarifa hiyo imekuja baada ya Jarida maarufu la kila mwezi la Uingereza la Economist, linalochambua masuala ya kiuchumi na kisiasa, katika toleo lake la Mei 2016, kudai katika taarifa yake kuwa tangu Rais Magufuli aingie madarakani, amezorotesha uchumi na ameifanya nchi ionekane kuwa haiwekezeki.

Habari hiyo pia iliandikwa na gazeti la hapa nchini la MwanaHalisi toleo la Mei 30 –Juni 5, mwaka huu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Meneja Uhusiano wa TIC, Daud Riganda alisema miradi hiyo inaonesha ongezeko la asilimia 20.31 ya miradi, ukilinganisha na kipindi cha miezi sita ambacho Rais Magufuli hakuwepo madarakani.

‘’Kuanzia Juni hadi Novemba mwaka jana, miradi ya uwekezaji ipatayo 458 yenye thamani ya dola za Marekani 5,727.29. Kati ya miradi hiyo, miradi 201 sawa na asilimia 44 inamilikiwa na watanzania, miradi 159 sawa na asilimia 35 inamilikiwa na wageni na miradi 98 (asilimia 21) inamilikiwa kwa njia ya ubia,’’ alisema Riganda.

Aliongeza kuwa, katika miradi hiyo ya uwekezaji iliyosajiliwa katika kipindi hiki, inatarajia kuzalisha ajira 55,970 wakati kwa miradi ambayo kabla ya Rais Magufuli kuingia madarakani ilitarajiwa kuzalisha ajira 39,361 na kuleta matokeo mengine kwa Watanzania.

Riganda alisema mitaji ya wageni ni Dola za Marekani milioni 7,196 na kwamba mitaji ya ndani ni sawa na Dola za Marekani milioni 2,015.8 huku katika miradi iliyopita, mitaji ya wageni ni Dola za Marekani milioni 4,020.3 na mitaji ya ndani ni Dola za Marekani milioni 1,706.9.

Alisisitiza kuwa uwekezaji umeongezeka hali inayoashiria imani waliyonayo wawekezaji kwa serikali, uwepo wa sheria za kuvutia uwekezaji, hali ya amani, usalama na sera rafiki na mazingira bora yaliyovutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Riganda alifafanua kuwa ripoti ya Dunia ya Uwekezaji iliyotolewa mwaka jana, inaonesha kuwa mitaji ya moja kwa moja ya uwekezaji kutoka nje (Foreign Direct Investment -FDI), ilipanda kwa asilimia 14.5 nchini.

Aidha, ripoti zinaonesha kwamba mwaka 2014, Tanzania iliingiza FDI nyingi ikilinganishwa na kipindi cha miaka mitatu. Kwa mujibu wa Riganda, katika kipindi hicho, Tanzania iliingiza FDI zenye thamani ya dola za Marekani milioni 2,142 ukilinganisha na dola za Marekani milioni 2,131 kilichoingizwa mwaka 2013.

‘’Mafanikio haya ya kuvutia na kuingiza mitaji ya moja kwa moja ya kigeni yamechangiwa na uvumbuzi wa gesi asilia katika miaka ya hivi karibuni hapa nchini. Tanzania ndiyo nchi inayoongoza katika Ukanda wa nchi za Afrika Mashariki kwa kuvutia na kuingiza mitaji ya moja kwa moja kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo,’’ alisisitiza Riganda.

Ofisa huyo pia alikiri kuwa ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ya mwaka huu, inayohusu ufanyaji biashara imeiweka Tanzania katika nafasi ya 139 kati ya nchi 189 ukilinganisha na nafasi ya 145 kati ya 189 waliyopata 2014.

Alieleza kuwa ripoti hizo hutolewa kulingana na vigezo mbalimbali ambapo kila kigezo hupewa alama kuanzia biashara ndogo na za kati hivyo hakuna uhusiano wowote kati ya vigezo hivyo na Rais Magufuli.

Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kadri inavyohitajika. Alisema pia uwekezaji unalindwa kisheria dhidi ya utaifishaji na kwamba jiografia nzuri inachangia biashara zifanyie kwa urahisi.

“’Pamoja na mambo mengine, tumeandaa ekari 63,000 eneo la Mkulanzi na tunakaribisha wawekezaji wa kilimo cha miwa na viwanda vya kuzalishia sukari… sekta ya kilimo inaongoza kwa uwekezaji na sekta inayofuata ni usindikaji wa mazao na bidhaa mbalimbali ambapo ajira 20,213 zitatolewa na fedha zilizowekezwa ni thamani ya Dola za Marekani milioni 912.25,’’ alisema.

Alisema sekta ya kilimo inatarajia kutoa ajira 507 na mitaji iliyowekwa ni dola za Marekani milioni 304 na kwamba idadi kubwa ya miradi iliyowekezwa ni ya Watanzania.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa alisisitiza kuwa waandishi wanatakiwa kuandika habari zenye ukweli kwamba serikali inasimamia ukuaji wa uchumi wa viwanda.

Zamaradi alisema kodi zinazopatikana zinatumika kustawisha maendeleo ya nchi na kueleza kuwa watawasiliana na Mwanasheria Mkuu wa serikali, kupata ushauri wa kisheria kulichukulia hatua jarida la The Economist.

Gazeti hilo la MwanaHalisi la Mei 30- Juni 5, mwaka huu, lilidai kuwa “Kwa mujibu wa The Economist, mambo makubwa kadhaa yaliyofanywa na Rais Magufuli yatachangia kwa kiasi kikubwa kudidimiza uchumi wa nchi.

Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa bidhaa zinazopitia bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani za Zambia, Congo DRC, Burundi na Malawi imesababisha kampuni nyingi za usafirishaji kusitisha matumizi ya bandari ya Dar.

Pia mwaka huu serikali ilianza kufukuza wafanyakazi wa kigeni wanaofanya kazi bila vibali sahihi wakiwemo maelfu ya walimu.



USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment