Thursday, 16 June 2016

Hii ndio kauli ya Yusuf Manji kuhusu barua yake kwa Rais Magufuli.

Mwenyekiti wa Kampuni za Quality Group Limited (QGL), Yusuf Manji amesema bado anasubiria majibu kutoka kwa Rais John Magufuli juu ya sakata la kuendeleza ufukwe wa Coco, maarufu Coco Beach uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam baada ya kumwandikia barua Desemba mwaka jana.

Manji alisema anatamani suala hilo limalizike kabla ya kuondoka rasmi katika kampuni hiyo mwezi ujao, na kwamba tayari alishamwandikia barua kiongozi huyo wa nchi juu ya usahihi wa mchakato wa zabuni wa kuendeleza eneo hilo la ufukwe wa Bahari ya Hindi.

Mfanyabiashara huyo anasema anashangazwa na baadhi ya viongozi wa Serikali kurudiarudia suala hilo na kusababisha kuwa maarufu kuliko hata Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, suala la Coco Beach ilikuwa ni sehemu ya biashara na kwamba zabuni hiyo walishinda baada ya kutimiza masharti yaliyokuwa yamependekezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, lakini cha kushangaza hali imekuwa tofauti.

Mfanyabiashara huyo alifikia hatua hiyo kufuatia Rais John Magufuli kutangaza eneo hilo liendelee kutumika na watu wa kawaida kwa kile alichosema kuwa kuna mfanyabiashara ambaye anatumia fedha kuwahonga baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo ili kumiliki eneo hilo.

Rais Magufuli ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa wafanyabiashara alisema; “Inanifadhaisha sana kuona mfanyabiashara tajiri akihonga maofisa kutumia vibaya fedha za umma kwa manufaa yake binafsi na wakazi kutoka mazingira duni wakishindwa kutumia ufukwe huo kuogelea na kuburudika.”

Hata hivyo, Manji alisema kuwa kampuni yake ilikuwa ikilihitaji eneo hilo kuliendeleza kwa ajili ya biashara na kuhudumia wananchi hivyo iwapo Rais ataridhia linyang’anywe licha ya kushinda zabuni na mahakamani, hawatakuwa na hatua nyingine ya kufanya.

Alisema Rais aliyasema yake na Mahakama ilishafanikisha ushindi wa awamu ya kwanza na Serikali baadaye ilikata rufaa na kwamba mtu yoyote akitaka kusoma kwa nini walishinda kesi ya awali, hukumu iliyotolewa inajieleza.

Manji alieleza kuwa ingekuwa eneo lile linahitajika kwa matumizi binafsi hata wangemwambia aliachie na achukue Jangwani angekubali, lakini kampuni isingekubali kwa sababu eneo lile lilitafutwa kwa ajili ya biashara na mbadala wowote huenda usiwavutie wanahisa.

 “Coco Beach siyo nyumbani kwangu na wala siyo sehemu ambayo lazima niwe nayo au nisiwe nayo. Ni sehemu ambayo kampuni ilihitaji kwa ajili ya uwekezaji,” alisema Manji.

“Wanahisa walitaka kuwekeza lakini iwapo halitapatikana, hawajatufungia milango ya kiuwekezaji kwa kuwa Coco Beach siyo sehemu moja tu duniani ya kuwekeza.”

Tayari QGL ilishaingia ubia na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) mwishoni mwa mwaka jana kutekeleza mradi wa Dola 250 milioni za Marekani (Sh537.5 bilioni) kuendeleza eneo la Bwawani, kwa kuikarabati hoteli hiyo na kujenga mji wa kisasa ambao utakuwa na huduma zote za kisasa katika visiwa hivyo.

No comments:

Post a Comment