Thursday 16 June 2016

Ripoti kamili kuhusu madudu mapya yaliopo katika bodi ya mikopo ya elimu ya juu.

RIPOTI ya kamati moja imeibua madudu zaidi katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).

Miongoni mwa madudu yaliyoibuliwa ni kuwepo kwa wanafunzi hewa zaidi ya 20 katika vyuo vya elimu ya juu, waliopoteza zaidi ya Sh milioni 56.2. Kamati hiyo iliundwa baada ya kusimamishwa kwa watendaji wakuu wa bodi hiyo.

Aidha, kamati hiyo imebaini kuwepo kwa wanafunzi wanaopata mikopo kutoka bodi hiyo na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar (ZHESLB), wengine 168 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na wanafunzi 919 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), walilipwa mikopo ya zaidi ya Sh bilioni tatu, ambayo haitambuliwi na vyuo na fedha hazikurudishwa.

Waziri wa Elimu, Sayansi Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema hayo jana wakati akitoa Ripoti ya Mkaguzi wa Ndani wa Serikali, aliyetakiwa kufanya ukaguzi wa hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu katika bodi hiyo, baada ya kubainika kuwepo kwa udhaifu.

Alisema katika ukaguzi huo, kati ya hoja 17 walizotakiwa kujibu ni hoja moja pekee ndiyo bodi walijibu kwa ufasaha huku nyingine 16 zikibaki. Hali hiyo ilionesha udhaifu mkubwa, ikiwemo faida inayopatikana kutokana na mikopo wanayopewa wanafunzi, kutumika katika kujilipa posho mbalimbali.

Alisema bodi hiyo imekuwa na matumizi yanayoongezeka kwa asilimia 90, huku faida ya Sh bilioni 31 waliyokopesha na kupatikana Sh bilioni tano, walitumia katika matumizi yao, badala ya kuzungusha kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi zaidi.

Alisema pia bodi hiyo wametumia fedha za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi kwa kijiidhinishia asilimia 30 ya mishahara kwa ajili kulipana posho za nyumba, asilimia 20 ya mishahara kwa posho ya mafuta na asilimia 10 kwa ajili ya posho ya matengenezo ya magari huku wakiwa na posho za usafiri kwa viwango vyao tofauti na Waraka wa Serikali.

Profesa Ndalichako alisema kumbukumbu za bodi, zinaonesha madeni kwa kiwango pungufu ya deni halisi na kutoa mfano wa wanafunzi 262 walinufaika na mikopo ya Sh bilioni 10.7. Lakini, kumbukumbu zinaonesha walitakiwa kurejesha Sh bilioni 5.5, ambayo ni pungufu ya karibu nusu.

Alisema pia wanafunzi 247 waliofanya marejesho ya mikopo yao ya awali kwa kiwango cha asilimia 25 na kulipa zaidi ya Sh milioni 270, hawajaingizwa kwenye orodha ya wanafunzi waliorejesha mikopo.

Profesa Ndalichako alisema pia imebainika kuwepo kwa udhaifu katika ufuatiliaji wa urejeshaji wa mikopo, inaonesha kuwa wanafunzi 105,202 waliokopeshwa kati ya mwaka 1994 hadi 2013, ambao mikopo yao iliiva na kutakiwa kurejesha zaidi ya Sh bilioni 712, hawajaanza kurejesha mikopo.

Pia ukaguzi umeonesha kuwa wanafunzi 2,619 wenye mikopo iliyoiva ya zaidi ya Sh bilioni 14.4, walikopeshwa wakiwa katika vyuo tofauti, lakini wanatumia namba moja ya kidato cha nne na kuonesha katika chuo cha kwanza walikopeshwa zaidi ya Sh bilioni 7.1 na chuo cha pili zaidi ya Sh bilioni 7.3.

Waziri huyo aliagiza baada ya wiki mbili, bodi kuhakikisha inatoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, kwani kuna uwezekano wa fedha kupotea, kwani wanaweza kulipa za chuo kimoja na siyo viwili ni vyema kujua kama kuna wanafunzi hewa na waliwekwa na nani.

Akizungumzia matatizo ya ukusanyaji madeni ya wanafunzi kwa kutumia wazabuni, ilibainika kuwa hakukuwa na sababu ya kuweka wazabuni ambao ni madalali katika kukusanya madeni hayo.

Alisema kulikuwa na wazabuni wanne, ambao walikuwa wakilipwa kwa kupewa kamisheni kulingana na ukusanyaji, jambo lililowafanya kuweka takwimu za uongo, wanufaika 462 wametambuliwa na wazabuni tofauti na kuwasilishwa HESLB wakiwa na kiasi kikubwa cha mikopo kuliko mikopo halisi zaidi ya Sh bilioni 2.8.

Alisema deni lilionesha ni zaidi ya Sh bilioni 3.6 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh milioni 828 lililofanya kamisheni kuwa kubwa kuliko ilivyostahili huku wakilipwa kamisheni kwa kutambua watu wanaofanana.

Alisema kazi ya kina inaendelea ya kubaini kuwepo kwa wanafunzi hewa katika elimu ya juu, ambapo wamebaini 20 wasiokuwepo katika chuo chochote, lakini wanalipwa mikopo kwa kufanya mchezo mchafu wa orodha inayopelekwa benki ya wanafunzi wanaotakiwa kulipwa mikopo.

Alisema kuna maelekezo ambayo siyo rasmi katika baadhi ya vyuo na yanayoenda benki na sasa wanafanya ukaguzi wa kina kupitia benki, ambapo awali kuna benki zilikuwa zikikataa kutoa miamala ya bodi, lakini sasa watakaokataa kuhakiki madai ya wanafunzi, watapiga marufuku mikopo kupitia benki hizo.

“Kuna wanafunzi wenye majina tofauti wanatumia akaunti namba moja, hili haliwezekani. Haiwezekani akaunti moja ikatumiwa na watu wawili. Ni vyema benki kutupa taarifa ya wanaotumia akaunti hizo, kwani tunafanya uhakiki kwa kushirikiana na Takukuru na baada ya wiki tatu tutatoa taarifa,” alisema.

Alisema wote waliohusika kufanya matumizi mabaya ya fedha hizo, wawe maofisa wa mikopo katika bodi au vyuoni au viongozi wa vyuo, kiama chao kimefika na ubadhilifu huo utaleta mtikisiko mkubwa, kwani yeyote aliyehusika na wizi huo, hatua kali za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa.

“Kitu kikubwa ni fedha zetu zilizotumika kinyume cha taratibu, zirejeshwe ili kusomesha watoto wa kitanzania kama ilivyokuwa imekusudiwa,”alisema.

Waziri huyo alisema baada ya kubaini hayo, serikali imechukua hatua za kutoa wiki mbili kwa bodi ya mikopo, kuwachukulia hatua mara moja wahusika wote na kuwapatia mashtaka wote waliosimamishwa za kinidhamu na kisheria. “Nilitamani kufuta kabisa bodi lakini nimeona niwaache wachunguze na kuchukua hatua stahili kabla sijaingilia kati,” alisema.

Pia aliwataka ndani ya muda huo, kutoa maelezo kuhusu wanafunzi 168 waliokopeshwa UDSM na 919 Udom lakini hawakutambuliwa na vyuo hivyo ; na hakuna ushahidi wa fedha hizo kurejeshwa Bodi ya Mikopo.

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment