Tuesday, 7 June 2016

Hizi ndio ndoa kongwe zaidi kuliko zote jijini Dar es salaam zapewa tuzo.

KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam limezitunukia tuzo maalumu ndoa kongwe zaidi ya tatu katika jimbo hilo. Ndoa hizo ni pamoja na ya Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Francis Mbenna na mkewe, Maura yenye miaka 61.

Wakongwe walioibuka washindi wa kwanza ni Emili Edward na Enocencia Lambert wenye miaka 64 na wa tatu ni Leonce Rutakyamirwa na Domitila miaka 56. Pamoja na ndoa hizo tatu, ndoa nyingine zenye miaka kati ya 30 hadi 39, 40 hadi 49, nazo zilitunukiwa tuzo za ndoa kongwe jimboni humo.
Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Eusebius Nzigilwa ndiye aliyekabidhi tuzo hizo zilizoandaliwa na Utume wa Familia ya Maridhiano, juzi jimboni humo na aliwataka wanandoa kuzingatia misingi ya imani, utu na upendo wa kweli kujenga ndoa imara ili kupata kanisa na taifa imara.
“Tumieni mitandao ya kijamii kuelimishana kuhusu umuhimu wa kuwa na familia bora ili ndoa zipone. Wapelekeni watoto ibadani nanyi muende, wekeni picha na vitu vitakatifu ndani ya nyumba zetu ili watoto wajifunze tangu utotoni,” alisema Askofu Nzigilwa.

Wakongwe hao watatu kwa nyakati tofauti, walisema kiini cha ndoa za sasa kuyumba na hata kuvunjika ni upendo bandia, unaotokana na wahusika kukutana kimjini mjini, bila kufahamiana vya kutosha na hawako tayari kuvumiliana madhaifu.

Mbenna na mkewe Maura, wanaotoka Parokia ya Changombe, wakizungumza na gazeti hili, walisema wao wamedumu kwa muda huo katika ndoa kwa kuwa walifahamiana muda mrefu kabla ya kuoana, walitoka kijiji kimoja na wazazi wao walifahamu tabia za kila familia.

“Msichana zamani kabla hujaolewa, wazee kadhaa waliitwa kumuasa kuhusu ndoa kwa kina. Lakini tulikuwa tunafahamiana tabia na Mbenna aliponichumbia, sikuona shida kwa kuwa nilimfahamu na familia yake niliifahamu vizuri na wao walitufahamu,” alisema Maura mwenye miaka 80.

Alisema anajivunia kuwa na mume mwenye kumcha Mungu kwa kuwa kwa kipindi chote cha maisha ya ndoa, wamewahi kugombana lakini ugomvi usiofika nje ya madirisha wala milango ya nyumba yao na hata siku moja mumewe hajawahi kumpiga.

Mbenna (86) alisema, “Nilipoamua kuoa nilijua ni kuishi pamoja, kuachana hakupo, upendo wa kweli ndio msingi wa kila kitu. Siku hizi vijana wanaoana kwa kuangalia mtu ana nini, wana ‘materialistic love’ (akimaanisha upendo bandia), wanakimbilia kuoa kwa kufuata mkumbo, waache hii tabia ndio maana hawadumu.”

Kwa mujibu wake, alibahatika kupata watoto saba, lakini wanne wametangulia mbele ya haki, na amebaki na watoto watatu, wawili wa kike na mmoja wa kiume. Ana wajukuu tisa na vitukuu wanne. Mshindi wa kwanza, Edward wa Parokia ya Mbezi Juu, alisisitiza kumcha Mungu kama chanzo cha maarifa ya kupata mke au mume mwema .

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment