Wednesday, 8 June 2016

Jeshi la Polisi lapiga marufuku maandamano,CHADEMA yatawanywa kwa mabomu

POLISI imepiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara, iliyokuwa imepangwa kufanywa na baadhi ya vyama vya siasa. 

Kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi, Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya, siku za hivi karibuni jeshi hilo limepokea taarifa kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa, vikitaka kufanya mikutano na maandamano, lakini wamepiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara kuanzia jana hadi hapo hali ya usalama itakapotengemaa.

Bila kutaja vyama vilivyowasilisha maombi, taarifa hiyo imesema polisi kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya habari, limebaini kuwa mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi.

“Aidha vyama vingine vya siasa vimeonesha dhamira ya kupinga kile ambacho kitasemwa na wapinzani wao,” alisema Mssanzya katika taarifa yake bila kufafanua vyama husika. Ingawa hakufafanua vyama vitakavyopinga kile kitakachosemwa na wapinzani wao, taarifa hiyo inatafsiriwa kuwa kulitegemewa kuwapo mikutano ya chama tawala na vya upinzani.

Taarifa hiyo ya Mssanzya iliendelea kusema kwamba vyanzo hivyo vya habari, vimebainisha kwamba upo uwezekano mkubwa wa kutokea vurugu baina ya makundi mawili ya kisiasa. Aliwataka wanasiasa kuacha mara moja kushinikiza wananchi kutotii sheria za nchi. Alisema hawatasita kumchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote au chama chochote cha siasa, kitakachokaidi agizo hili.

Aidha, jeshi hilo limewataka wananchi kuwa makini na wanasiasa wenye lengo la kutaka kuvuruga amani ya nchi. Mssanzya aliwasihi wananchi waendelee kushirikiana katika kujenga umoja wa nchi.

ACT yalia na polisi.
Wakati huo huo, Chama cha ACT Wazalendo kimelaumu uamuzi huo wa polisi wa kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Chama hicho kilisema uamuzi huo wa polisi, unatokana na kuzinduliwa kwa mpango wao wa ‘Operesheni Linda Demokrasia’ kumpa fursa Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto na wabunge wengine wa upinzani, waliosimamishwa bungeni kuwaeleza wananchi juu ya kile kinachodaiwa ni kuminywa kwa demokrasia bungeni.

“Mikutano ya ‘Operesheni Linda Demokrasia’ inayoratibiwa na chama chetu ilipangwa kufanyika kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya na Morogoro, mpaka sasa umeshafanyika mkutano mmoja jijini Dar es Salaam,” ilisema taarifa ya Katibu Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu.

Chama hicho kilituhumu Jeshi la Polisi kuwa limeminya haki ya kisheria ya vyama kufanya mikutano. Kimesema kinawasiliana na wanasheria wake kupata tafsiri ya kimahakama ya uhalali wa polisi kuzuia mikutano ya vyama vya siasa ambayo inatambuliwa na kulindwa na katiba.

CCM ilishajiandaa
Amri hiyo ya polisi imekuja siku moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa msemaji wake, Christopher Ole Sendeka kukaririwa na waandishi wa habari, akishutumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Alisema chama hicho cha upinzani, kinataka kwenda kuishitaki serikali kwa wananchi kwa hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa kuziba mianya ya rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.

Sendeka alisema atahakikisha kila watakapotoka (vyama vingine) kufanya mikutano yao, ataingia na Watanzania watapima kati ya kauli ya wanaowakilisha mafisadi wanaokwepa kodi, watumishi wavivu na watendaji wanaohakikisha kodi ya Watanzania inatumika vizuri.

“Kama hoja zao ni hizi nawaonea huruma sana, wanafikiri kama Watanzania watawaunga mkono, nina hakika si tu kwamba hawatawaunga mkono, bali Watanzania wataendelea kuwashangaa na chati yao itashuka,” alisema.

Sendeka alisema ni jambo la ajabu kuona wakati serikali inashughulika na walanguzi wachache, ambao wamekuwa wakilikosesha taifa mapato, kikundi cha watu wachache wanakwenda kukisemea kikundi hicho na kuitaja Tanzania kama nchi ya kifashisti na kidikteta jambo ambalo si sawa.

Mabomu yatawanya Chadema
Wilayani Kahama, Polisi kwa kushirikiana na wa Mkoa wa Shinyanga, jana waliwasambaratisha kwa kutumia mabomu ya machozi na gari la maji ya kuwasha wafuasi na viongozi wa juu wa Chadema, waliokuwa wakitaka kufanya mkutano mjini hapa kinyume cha sheria.

Tukio hilo lilitokea saa 7 mchana kwenye viwanja vya CDT wakati viongozi hao wa ngazi za juu wa chama hicho, walipokuwa wakitaka kufanya mkutano wa kufungua kampeni ya “Operesheni Okoa Demokrasia Kanda ya Ziwa. Katika tukio hilo, viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, magari yao yalimwagia maji hayo ya kuwasha baada ya kuingia katika viwanja hivyo kuanza mkutano wao huo.

Hata hivyo, baada ya kutokea hali hiyo ya sintofahamu, wananchi walikimbia ovyo kukimbia mabomu ya machozi yaliyokuwa yakipigwa na askari wa Jeshi la Polisi Kahama kwa kushirikiana na wale waliopo mjini Shinyanga, waliokuja kwa ajili ya kuongeza nguvu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo, Mbowe alisema kitendo walichofanyiwa na Polisi, sio cha kiungwana na kuwa taarifa za kufanya mkutano waliokuwa nazo tangu juzi, hivyo haiwezekani kuwazuia jana.

Mbowe alisema hawataacha kufanya mikutano yao hiyo, akidai haki ya kila mwananchi kupata taarifa na kwamba kwa sasa wanakaa vikao vya ndani, kujadili suala hilo na ikibidi watalifikisha mahakamani kwa fujo walizofanyiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange alisema walisitisha mkutano huo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo zile za kiintelejensia, walizokuwa nazo kuhusu mkutano huo.



USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment