HATIMAYE kitendawili cha lini makabidhiano ya kijiti cha Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yatafanyika, kimeteguliwa baada ya chama hicho tawala nchini kutangaza tarehe rasmi ya Mkutano Mkuu Maalumu wa kukabidhiana hayo.
Hatua ya kutangazwa kwa tarehe rasmi ya mkutano huo imekuja bada ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi jana katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya Chama, Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi hizo, Msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka alisema Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho unatarajiwa kufanyika Julai 23, mwaka huu.
Alisema uamuzi wa kufanyika kwa mkutano huo imefikiwa baada ya kikao cha Kamati Kuu kuridhishwa na maandalizi yanayoendelea mjini Dodoma.
“Lengo kuu la Mkutano Mkuu huo Maalumu ni kukabidhiana kijiti cha uongozi wa juu wa chama chetu kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kwenda kwa Rais wa sasa Dk John Magufuli kama ulivyo utamaduni wa CCM,” alisema Sendeka.
Alisema mkutano huo ambao utajumuisha wajumbe 2,l430 kutoka nchi nzima utatanguliwa na vikao vya Sekretarieti, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa na kwamba mkutano huo utakuwa ni wa siku moja.
Aidha, alisema mkutano huo utahudhuriwa na wageni kutoka nje ya nchi, mabalozi, waasisi wa chama hicho, viongozi wakuu waastafu pamoja na vyama vyote vyenye usajili wa kudumu nchini.
“Mkutano huu unatarajiwa kuendeleza utamaduni wa CCM wa kukabidhiana kijiti cha uenyekiti kutoka kwa Kikwete kwenda kwa Rais Magufuli kama ilivyokuwa huko nyuma,” alisema.
Sendeka alifafanua kuwa kwa matakwa ya Katiba ya chama hicho, Rais Magufuli anatakiwa kupata nusu ya kura zote.
Kutangazwa kwa tarehe hiyo kumemaliza sintofahamu iliyokuwepo ya madai ya kuwepo kwa mgogoro ndani ya chama hicho katika mchakato wa makabidhiano ya kijiti cha uenyekiti, jambo ambalo lilikuwa likipingwa na chama hicho.
Kikwete ambaye aliingia madarakani kuiongoza Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Nne Desemba 21, mwaka 2005 na kukabidhi madaraka kwa Rais Magufuli Novemba 5, mwaka jana, aliutwaa Uenyekiti wa CCM Juni 2006 kutoka kwa mtangulizi wake, Benjamin Mkapa aliyekuwa pia Rais wa Awamu ya Tatu kati ya mwaka 1995 na 2005.
USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE
No comments:
Post a Comment