Monday 13 June 2016

Waziri Mkuu atoa ufafanuzi wa sakata la uhaba wa sukari na atangaza kiwango hiki ndio kiwe bei ya sukari nchini.

Majaliwaaa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kwamba Serikali inaendelea na jitihada za kuondoa tatizo la uhaba wa sukari nchini. Amesema jumla ya tani 20,000, zilisambazwa juzi katika maeneo mbalimbali nchini.


Taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, jijini Dar es Salaam ilisema Waziri Mkuu alisema shehena nyingine ya tani 35,000 inatarajiwa kusambazwa hivi karibuni katika kanda zote nchini. Hivyo, aliwataka wafanyabiashara watakapoipokea, kuiuza kwa wananchi bila ya kuificha na bei isizidi Sh 2,200.

Alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na mashehe na viongozi wa Kamati ya Amani ya mkoa wa Dar es Salaam, alipowaalika katika futari aliyoiandaa nyumbani kwake.

Alisema tayari viwanda vimeanza kufunguliwa na tani 300 zilizotoka katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera, zitasambazwa mkoa wa Kigoma katika wilaya za Kakonko, Kibondo, Kasulu, Uvinza na Kigoma ili kutosheleza maeneo hayo.

Hata hivyo, aliwataka maofisa biashara katika halmashauri zote nchini, kuendelea kufuatilia katika maduka ili kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana na hakuna mfanyabiashara atakayeificha.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wafanyabiashara kote nchini kutopandisha bei za vyakula katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Akizungumza kuhusu tabia za baadhi ya wafanyabiashara wanaopandisha bei za bidhaa, hasa vyakula katika kipindi hiki cha Mfungo, aliwataka kumuogopa Mwenyezi Mungu kwa sababu kitendo hicho, kinawapa wafungaji wakati mgumu.

“Kufunga Ramadhani si jambo la anasa, si matashi binafsi, bali ni jambo la kiimani, hivyo tusipandishe bei ya bidhaa kwa lengo la kuwaadhibu Waislamu kwa sababu tu wamefunga.

“Katika Quran surat Baqarah aya ya 183 inasema kwamba enyi mlioamini imefaradhishwa kwenu kufunga kama walivyoamrishwa kufunga kwa waliopita kabla yenu ili muwe wacha Mungu, hivyo hatuna budi kufunga,” alisisitiza.

Alisema tabia hiyo si nzuri na imekuwa ikijitokeza mara kwa mara unapofika wakati wa mfungo kwa wafanyabiashara kuamua kupandisha bei. Aliwataka waache tabia hiyo, kwani Serikali haitawavumilia na atakayethubutu, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

No comments:

Post a Comment