Saturday, 23 July 2016

Kamati Kuu ya CHADEMA kukutana kwa dharura Dar es Salaam kujadili mambo haya.


Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), itakutana kwa dharura, jijini Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe, ambapo pamoja na masuala mengine, itapokea taarifa na kujadili hali ya siasa nchini.

Katika siku za hivi karibuni, taifa limekuwa likipitia katika majaribu makubwa, ikiwa ni pamoja na uvunjifu mkubwa wa sheria na taratibu za kuongoza nchi unaofanywa waziwazi na mamlaka za juu/viongozi waandamizi wa nchi kupitia kauli na matendo mbalimbali kiasi cha kuwashtua Watanzania ambao wangependa kuona nchi yao ikiendeshwa katika misingi ya uwajibikaji wa kisheria na demokrasia.

Katika kikao hicho cha siku mbili, Julai 23-24, mwaka huu, Kamati Kuu pia itapokea taarifa na kujadili kabla ya kufanya maamuzi kuhusu mipango mbalimbali inayoendelea ya kukipanga chama ili kiendelee kufanya shughuli zake kwa ufanisi hususani kinapokwenda kuimarisha misingi kuanzia ngazi ya kitongoji nchi nzima, kupitia usimamizi wa kanda 10 za chama.

Imetolewa  na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Habari CHADEMA

No comments:

Post a Comment