TANZANIA imeuhakikishia Umoja wa Afrika (AU) kwamba itaendelea kufanya kazi kwa karibu na nchi wanachama wa umoja huo, kujadili changamoto za kiusalama zinazolikabili bara la Afrika, kwa njia ya mazungumzo na upatanishi, kama inavyoelekeza Katiba ya AU.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alitoa kauli hiyo wakati akichangia mada kuhusu hali ya amani na usalama katika bara la Afrika, kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika mjini Kigali, Rwanda.
Samia alisema Tanzania inasikitishwa na inalaani matukio ya uvunjifu wa amani yanayoendelea kujitokeza katika baadhi ya nchi za Afrika kiasi cha kutishia usalama wa raia.
Alielezea mauaji ya Hafsa Mossi aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na Waziri wa zamani wa Burundi na mapigano ya hivi karibuni Sudan Kusini ambako mamia ya raia wasiokuwa na hatia waliuawa na wengine maelfu wameachwa bila makazi, kwamba ni mwendelezo wa uvunjifu wa amani katika nchi hizo.
Aliwataka wadau husika katika nchi za Burundi na Sudan Kusini kushiriki kikamilifu katika mazungumzo yanayoendelea kwa kuwa hiyo ndiyo njia muafaka ya kuleta amani, usalama na utulivu wa kudumu katika nchi zao.
Aidha, aliiomba Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuisaidia Sudan Kusini kutafuta ufumbuzi wa kudumu katika mgogoro ulioikumba nchi hiyo.
Akichangia kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Makamu wa Rais alisema Tanzania kwa ujumla inaunga mkono msimamo wa Afrika wa kuwa na viti viwili katika baraza hilo na kura ya turufu bila ya masharti yoyote.
No comments:
Post a Comment