Thursday 18 August 2016

Hii ndio idadi ya Wanafunzi Hewa waliobainika katika Shule za Sekondari Mkoani Simiyu.

Baada ya kufanya uhakiki wa Wanafunzi Uongozi wa Mkoa wa Simiyu umebaini uwepo wa wanafunzi hewa 2331  katika shule za Sekondari za Mkoa huo.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka wakati alipozungumza na Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata mara  baada ya kuwakabidhi Vishikwambi (Tablets) vilivyotolewa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la EQUIP Tanzania kwa ajili ya utunzaji wa Takwimu muhimu za Sekta ya Elimu,.

Mtaka amesema kati ya Halmashauri sita za Mkoa huo, Ni Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi  tu ambayo haina wanafunzi hewa wakati Halmashauri ya Wilaya ya Busega ikiwa na wanafunzi hewa  110, Itilima  2137, Maswa 14, Meatu 125 na Halmashauri ya Mji wa Bariadi 439.

Kufuatia kuwepo kwa wanafunzi hewa Mkuu wa Mkoa huo amesema, Serikali Mkoani humo imepanga kufanya mabadiliko ya Wakuu wa Shule za Sekondari katika Mkoa mzima, wakati taratibu za kinidhamu zikiendelea kwa wakuu wa shule  waliotoa takwimu za uongo za wanafunzi katika shule zao, wakati kwa upande wa shule za Msingi, mabadiliko yatafanyika baada ya kumaliza mtihani wa darasa la saba.

Mtaka amesema kabla ya uteuzi wa wakuu wa shule na walimu wakuu utafanyika upekuzi (vetting) kwa wale watakaopendekezwa ili kujiridhisha kama wahusika wana sifa na uwezo wa kuendesha shule na kusimamia fedha za Serikali zinazopelekwa shuleni kwa ajili ya kugharama elimu ya bila malipo. 
 
“ Serikali inaendelea kupelekea fedha moja kwa moja katika akaunti za shule, kwa hiyo mkuu wa shule au mwalimu mkuu ni afisa masuuli katika shule yake. Ipo haja kwa sisi kujiridhisha kama Serikali kuwa anayeteuliwa kushika nafasi ya kuongoza shule ana uwezo na sifa  ya uadilifu. Sitakuwa tayari kuona katika mkoa huu kuna walimu wakuu wazoefu wa kula fedha za Serikali na wakaendelea kuongoza shule”alisema Mtaka.


USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment