Wednesday 3 August 2016

Huu ndio Msimamo wa Tundu Lissu kuhusu kesi inayomkabili dhidi uchochezi.

Baada ya kesi yake kuahirishwa jijini Dar es Salaam kuwa suala hilo halikubaliki kwa kuwa sheria inawaruhusu kufanya mikutano popote. 

“Mbona huniulizi kama Magufuli yuko sahihi anaposema kila mmoja akafanye mikutano kwenye kajimbo kake?” Lissu aliwauliza waandishi nje ya Mahakama ya Kisutu akionekana kutaka kuzungumzia suala hilo baada ya kuulizwa swali tofauti. 

“Sheria ya Tanzania inasema chama kilichopata usajili wa kudumu kina haki ya kufanya mikutano ya hadhara mahali popote,” alisema.

Alisema chama chenye usajili kina haki kufanya mikutano na kwamba Rais Magufuli alitangaza zuio hilo bila ya kusoma sheria. 

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya nchi hii na sheria zake zote, hana mamlaka yoyote ya kusema lolote au kufanya lolote kuhusiana na mikutano ya hadhara,” alisema. 

“Mtu anayetambuliwa na sheria kuhusiana na mikutano ni OCD peke yake.” 

Lissu alisema kuweka mipaka hiyo kwa wanasiasa kufanya shughuli zao kwenye maeneo waliyoshinda tu, itawanyima haki viongozi ambao vyama vyao havikupata ushindi, akitoa mfano wa Augustine Mrema, ambaye ni mwenyekiti wa TLP na John Cheyo (mwenyekiti UDP), kufanya shughuli za siasa. 

Lissu pia alizungumzia uamuzi wao wa kutangaza mikutano ya hadhara nchi nzima wakati wakiwa wamefungua kesi kutaka tafsiri ya Sheria ya Vyama vya Siasa. 

“Kesi mahakamani, maisha hayasimami. Hatuachi kuwa chama cha siasa, hatuachi kuwa na haki zetu kama vyama vya siasa. Haki zetu zinabaki palepale,” alisema Lissu alipoulizwa sababu za Chadema kutangaza mikutano ya hadhara kabla ya uamuzi wa kesi yao haujatoka.

 “Na kwa mujibu wa sheria, na sheria yenyewe ni ya Vyama vya Siasa, ni kwamba vyama vya siasa vina haki ya kufanya maandamano na mikutano ya hadhara kwa mujibu wa sheria. 

“Kwa hiyo tutafanya maandamano na mikutano nchi nzima, si kwa sababu tumefungua kesi tu, bali kwa sababu tuna haki kwa mujibnui wa sheria za Tanzania kufanya maandamano na mikutano, kama alivyo na haki mwenyekiti mpya wa CCM bwana Magufuli, kama alivyo na haki bwana ole Sendeka (msemaji wa CCM), kama alivyo na haki kiongozi wa chama chochote kilichosajiliwa.” 

Alisema hawawezi kuacha kutumia haki yao ambayo ipo kisheria kwa sababu tu Mahakama haijatoa uamuzi. 

Kesi ya uchochezi 
Jana, katika kesi nayomkabili Lissu, upande wa mashtaka umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mshtakiwa huyo alikiri mbele ya polisi kutenda kosa la kutoa maneno ya uchochezi. 

Wakili wa Serikali, Bernard Kongola alisema hayo wakati akimsomea Lissu maelezo ya awali ya kesi ya kutoa maneno ya uchochezi. 

Hata hivyo, Lissu aliyakana maelezo hayo na badala yake katika maelezo hayo alikubali utambulisho wake tu, yaani jina lake na wadhifa wake kuwa ni mbunge. 

Baada ya kusomewa maelezo hayo na kukana mashtaka hayo, Hakimu Dk Yohana Yongolo anayesikiliza kesi hiyo aliiahirisha hadi Agosti 24 wakati upande wa mashtaka utakapoanza kutoa ushahidi. 

Akimsomea maelezo ya awali, Wakili wa Serikali aliieleza mahakama kuwa Lissu alitenda kosa la kumuita Rais Magufuli kuwa ni dikteta Juni 28, 2016 katika eneo la mahakama hiyo, alikokuwa amekwenda kwenye kesi nyingine ya jinai. 

Wakili Kongola alinukuu maneno hayo kuwa alisema: “Mamlaka ya Serikali mbovu ya kidikteta uchwara yanapaswa kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote. Huyu dikteta uchwara lazima apingwe kila sehemu kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga, nchi itaingia kwenye giza nene.” 

Wakili Kongola alisema kuwa Juni 29, 2016, mshtakiwa huyo alikamatakwa akiwa nyumbani kwake Tegeta Kibaoni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam na kwamba alipohojiwa alikiri kutamka maneno hayo. 

Jana nje ya mahakama, Lissu aliwashukuru wafuasi waliofurika kushuhudia kesi hiyo akisema ni ishara nzuri na kwamba watamaliza kesi zote zinazowakabili kwa kufurika kwa wingi mahakamani na hivyo kuwa kero.


No comments:

Post a Comment