Monday 15 August 2016

Huu ndio wosia mzito aliouacha Aboud jumbe kabla ajafariki.

WOSIA ulioachwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aboud Jumbe Mwinyi umezidisha simanzi katika kifo chake kilichotokea Dar es Salaam jana.
Wakati wa uhai wake, Jumbe (96) aliagiza maziko yake kuwa ya kawaida kwa mujibu wa misingi ya dini ya Kiislamu, ingawa familia yake imesema hatua hiyo haiwazuii viongozi wa serikali kuhudhuria shughuli nzima za mazishi yake.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa Jumbe, Mjimwema Kigamboni, Dar es Salaam jana, msemaji wa familia, mtoto wa marehemu, Mustafa Aboud Jumbe pamoja na kueleza kuwa marehemu atazikwa katika makaburi ya Migombani, mjini Unguja Zanzibar leo, alisema sharti lililowekwa na kiongozi huyo la maziko yake kuwa ya kawaida na ya misingi ya dini, litazingatiwa kama alivyoagiza wakati wa uhai wake.

Historia yake kisiasa.
Jumbe alishika madaraka ya kuongoza Zanzibar katika mwaka 1972 baada ya kuuawa kwa Abeid Amaan Karume ambapo Baraza la Mapinduzi kwa kauli moja lilimchagua kushika wadhifa huo wa Rais wa Zanzibar.
Kutokana na kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar katika mwaka 1984, Jumbe alilazimika kujiuzulu pamoja na viongozi wengine akiwemo Waziri Kiongozi Ramadhan Haji Faki na hivyo kupoteza nyadhifa zote, ikiwemo Makamu wa Rais wa Muungano na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Jumbe atakumbukwa kwa mambo mengi akiwa ni mmoja ya viongozi walioshirikiana na Mwalimu Nyerere kuzaliwa kwa CCM mwaka 1977 katika Uwanja wa Amaan Zanzibar.
Kabla ya kuzaliwa kwa CCM, Jumbe alikuwa Rais wa Chama cha ASP ambapo ushawishi wake mkubwa ndiyo uliosababisha kuunganishwa kwa vyama hivyo na kuzaliwa kwa CCM, ikiwa ni moja ya juhudi za kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika kuimarisha demokrasia na sauti za wananchi kusikika, Jumbe alianzisha chombo cha kutunga sheria ambacho alikiita Baraza la Wawakilishi. Baraza la Wawakilishi liliasisiwa katika mwaka 1979 kwa kuanzia viongozi kutoka katika Wilaya za Unguja na Pemba kwa kuzishirikisha jumuiya za chama ikiwemo Umoja wa Vijana, Wazazi, Ushirika na Umoja wa Wanawake (UWT).
Huo ndiyo mchango mkubwa wa Jumbe katika kuanzisha chombo cha Baraza la Wawakilishi ambalo aliliita ngome ya wananchi katika kusikiliza maoni yao.
 Ujumbe wa Rais Magufuli
 Rais Magufuli alisema “Nimeshitushwa sana na kifo cha Mzee wetu Mheshimiwa Aboud Jumbe, kwa hakika Tanzania imepoteza mtu muhimu ambaye katika kipindi cha uongozi wake, alitoa mchango mkubwa wa kuipigania na kuijenga Tanzania tunayoiona leo.”


USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment