Wednesday 17 August 2016

Mkurugenzi wa Wilaya ya Gairo aangua kilio baada ya kuhojiwa mbele ya kamati ya Bunge.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Agnes Mkandya jana alijikuta akiangua kilio wakati akihojiwa mbele ya Kamati ya Bunge ya LAAC, kutokana na kuulizwa maswali mfululizo ya ubadhirifu wa fedha kwenye halmashauri hiyo.

Mkandya alijikuta katika wakati mgumu wakati akijibu maswali yaliyohusu ubadhirifu, hatua iliyofanya kuanza kulia na kumlazimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ngombale, kumtaka kuwa mtulivu wakati akijibu maswali.

Tukio hilo lilitokea wakati Mkurugenzi huyo, alipoulizwa swali na Mbunge wa Viti Maalum, Leah Komanya (CCM) ambaye ni mjumbe wa Kamati hiyo, aliyetaka majibu kuhusu ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri ya Gairo.

Akijibu, Mkurugenzi huyo alisema amewasimamisha kazi wakuu tisa wa idara na halmashauri hiyo kutokana na ubadhirifu uliokithiri. Hata hivyo, wakati wabunge wakiendelea kusikiliza maelezo zaidi, Mkurugenzi huyo alishindwa kuendelea kujibu na badala yake kuangua kilio.

Kutokana na kitendo hicho, Mwenyekiti wa Kamati alimtaka Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri kujibu swali hilo, lakini naye aliposimama alisema wana muda mfupi tangu wakabidhiwe madaraka, hivyo inakuwa vigumu kuweza kujibu maswali yote.

Kutokana na majibu hayo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo alimuinua Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dk John Ndunguru kujibu swali hilo, ambapo aliposimama alisema viongozi wengi ni wageni na watajitahidi kufuata maagizo watakayopewa.

Katika maelezo ya swali, Mbunge Komanya alisema Halmashauri ya Gairo imekuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha kwa kutumia karatasi za nukushi (carbon slip), hivyo kuikosesha serikali mapato na kumuagiza mkurugenzi huyo kutoa majibu.

Akijibu hoja hiyo, mkurugenzi huyo alisema suala la wizi wa aina hiyo lilijitokeza ambapo walikamata mtendaji mmoja na sasa wanaendelea na kazi ya kufunga Mashine za Kielektroniki za Kukusanya Mapato (EFD’s) huku Kampuni ya Simu (TTCL) ikifanya taratibu za kuwaunganisha.

“Mimi nilikuwa natoa angalizo, nataka Mkurugenzi ajibu kama nilivyouliza, sitaki maelezo mengi,” alisema Komanya na kumfanya mkurugenzi huyo kuangua kilio na kuchukua kitambaa cha kujifuta machozi.

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment