Monday, 8 August 2016

Rais Magufui atoa kauli hii kwa watanzania akiwa Chato Mkoani Geita.

RAIS John Magufuli ametembelea msikiti na makanisa yaliyopo Chato mjini mkoani Geita na kuendelea kuwasihi Watanzania kuombea amani na utulivu katika nchi, bila kujali tofauti za dini, makabila na kanda wanazotoka.

Rais alitoa ujumbe huo mara baada ya kusali ibada ya Jumapili katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria Parokia ya Chato. Baadaye alitembelea Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Stephano Parokia ya Chato, Kanisa la African Inland Church la Chato na kumalizia katika Msikiti wa Omar Bin-L-Khattab wa Chato.
Rais Magufuli alisema pamoja na Watanzania wote kuungana kuombea amani na utulivu, pia hawana budi kutekeleza kwa vitendo maandiko matakatifu ya Biblia yasemayo “Asiyefanya kazi na asile” kwa kuhakikisha kila mmoja anachapa kazi kwa juhudi na maarifa ili kuharakisha maendeleo ya Taifa.
“Ndugu zangu nawashukuru sana, muendelee kuliombea taifa hili, taifa letu ni la umoja, sisi wote ni Watanzania, tuendelee kumuomba Mola wetu, kudumisha amani yetu, kujenga umoja wetu kwa dini zote, makabila yote na vyama vyote, kwa sababu Mola wetu anatupenda sisi sote,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, baada ya kuwasalimu waumini wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Parokia ya Chato, Rais Magufuli aliendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo jipya la kanisa hilo, ambapo Sh milioni moja zilikusanywa papo kwa hapo.
Tayari Rais Magufuli alishachangia ujenzi huo kwa kutoa Sh milioni moja Aprili 3, mwaka huu.
Alitoa wito kwa watu mbalimbali, kujitokeza kuchangia ujenzi wa kanisa hilo. Katika Msikiti wa Omar Bin-L-Khattab na makanisa ya Anglikana na African Inland, Rais Magufuli alichangia Sh milioni tano kwa kila moja kwa ajili kuendeleza na kukarabati majengo.

No comments:

Post a Comment