Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa 32 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Nchini (ALAT) ambao utafanyika mwishoni mwa mwezi ujao mkoani Musoma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Makamu Mwenyekiti wa ALAT Bw. Stephen Mhapa amesema kuwa, katika mkutano huo wanatarajia Rais Magufuli kuwa mgeni rasmi ili kufikia malengo ya mkutano huo.
“Tumeamua kumuomba Mheshimiwa Rais kuwa mgeni rasmi kwa ajili ya kupata matunda mema ya mkutano huo kutokana na kauli mbiu yake ya Hapa Kazi Tu ili kuendana na kasi hiyo katika kuleta mendeleo na uongozi bora nchini,” alisema Bw. Mhapa.
Aidha Bw. Mhapa amesema kuwa uzinduzi wa mkutano huo utaendana na ukabidhishaji wa zawadi kwa mshindi wa shindano la Halmashauri bora kwa mwaka 2016 ambapo mshindi atayechaguliwa na wananchi kwa wingi atakabidhiwa Trekta yenye thamani ya shilingi milioni 56 ili kuinua shughuli za kimaendeleo.
Mbali na hayo Bw. Mhapa ameongeza kuwa mkutano huo utadhaminiwa na Benki ya NMB kwa kupokea kiasi cha shilingi milioni 206 ambazo milioni 56 zitatumika kugharamia zawadi na milioni 150 kugharamia mkutano huo.
Kwa upande wa Mkuu wa Kitengo cha Biashara za Serikalini kutoka benki ya NMB Bi. Domina Feruzi amesema kuwa wameamua kufadhili mkutano huo ili kurahisisha shughuli za kimaendeleo na kupata uongozi bora kwa faida ya watanzania.
“Tumeamua kudhamini mkutano huo ili kuweza kurahisisha shughuli za kimaendeleo na kupata viongozi bora kwa kupitia mashindano ya Halmashauri Bora mwaka 2016,”amesema Bi. Domina.
ALAT imekuwa na utaratibu wa kutoa zawadi kwa Halmashauri bora kwa mwaka wa pili sasa ambapo imesaidia Halmashauri nyingi kufanya vizuri katika ukusanyaji mapato na uboreshaji wa miundo mbinu na mazingira kwa ujumla.
USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE
No comments:
Post a Comment