Wednesday, 7 September 2016

Huu ndio ujumbe aliopokea Rais Magufuli kutoka kwa Rais Salva Kiir na Pierre Nkurunziza.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Burudi uliowasilishwa kwake na Aime Laurentine Kanyana Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na IKULU
Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit amemtumia ujumbe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akimuarifu kuwa hali ya usalama katika nchi hiyo imeanza kutengemaa.

Rais Salva Kiir Mayardit amewasilisha ujumbe huo kupitia kwa Mjumbe wake Maalum Mhe. Aggrey Tisa Sabuni ambaye pamoja na kuwasilisha ujumbe huo amesema Sudani Kusini imekamilisha nyaraka za azimio la kuridia mkataba wa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao umewasilishwa jana tarehe 05 Septemba, 2016 katika makao makuu ya Jumuiya Jijini Arusha.
Mhe. Aggrey Tisa Sabuni amesema Sudan Kusini ipo tayari kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi ikiwemo biashara na uwekezaji na kwamba ni matumaini yake kuwa itapata ushirikiano mzuri.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na taarifa za kutengemaa kwa hali ya amani nchini humo na kwamba ni matarajio yake kuwa Sudan Kusini itajikita katika maendeleo ya wananchi wananchi wake.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza ulioletwa na Mjumbe Maalum wa Rais huyo Mhe. Aime Laurentine Kanyana.

Katika ujumbe huo Rais Nkurunziza amesema hali ya Burundi ni shwari na kwamba wananchi wa Burundi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

Kwa upande wake Rais Magufuli amesema Tanzania yenye wakimbizi takribani 200,000 wa kutoka Burundi inafurahishwa na taarifa za kuwepo hali ya amani nchini humo.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

USISAHAU KULIKE NA KU-SHARE NA KU-LIKE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPO ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment