Friday, 16 September 2016

Milioni 123 yasababisha Timu za Ligi kuu kuigomea TFF.

Image result for malinzi
Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na ule wa Bodi ya Ligi (TPLB), hivi karibuni umekumbana na balaa kubwa kutoka kwa viongozi wa timu zinazoshiriki  Ligi Kuu Bara msimu huu.


Balaa hilo si jingine bali ni uamuzi mzito uliofikiwa hivi karibuni na viongozi wa timu hizo wakitaka wapewa fedha zao zote za haki ya matangazo ya Ligi Kuu Bara ambazo zimebakia ili ziweze kuzisaidia katika mbio zao za kuwania ubingwa wa ligi kuu msimu huu.



Viongozi hao wameitaka TPLB kuhakikisha unawapatia fedha hizo takriban shilingi milioni 123 kwa kila timu kabla ya kumalizika kwa mwezi Oktoba na hawataki tena kuendelea na mfumo uliokuwa ukitumika hapo awali wa kupewa kwa awamu.
 

 Habari za kuaminika kutoka ndani ya TFF zimedai kuwa, sababu kubwa iliyosababisha yote hayo ni baada ya kuibuka kwa taarifa kuwa TPLB ilikuwa na mpango wa kutaka kubadili mfumo wa utoaji wa fedha jambo ambalo liliwashtua viongozi hao.


“TPBL ilikuwa katika mchakato wa kutaka kuzitoa fedha hizo kwa mtindo wa asilimia ambapo timu inayofanya vizuri ligi kuu ndiyo iwe inapata fedha nyingi na ile inayofanya vibaya inapata kiasi kidogo.



“Lengo lake kubwa lilikuwa ni kutaka kuongeza ushindani lakini viongozi wa timu hizo wakakataa mfumo huo na wanataka wapewe fedha zao zote zilizobakia ambazo ni kama milioni 123 kwa kila timu, ili kuepusha malumbano, TPLB imekubali kuwapatia fedha hizo hivyo,” kilisema chanzo hicho cha habari.



Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Boniface Wambura ili azungumzie suala hilo hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita tu bila ya kupokelewa.


Katibu Mkuu wa Majimaji ya Songea, Zacharia Ngalimanayo ambaye alitajwa kuwa mmoja wa viongozi wa timu hizo waliokuwa mstari wa mbele kudai fedha hizo ili aweze kuthibitisha juu ya suala hilo, naye bila ya kusita alisema:



“Ni kweli tumetaka tupewe fedha zetu hizo na hatutaki mambo mengine. Tumefikia uamuzi huo kwa sababu tumeona kuwa endapo utaanza kutumika mfumo wa asilimia basi sisi ambao timu zetu ni dhaifu tutapunjika na zitakazokuwa zikifaidi ni  Simba, Yanga na Azam,” alisema Ngalimanayo.


USISAHAU KULIKE NA KU-SHARE NA KU-LIKE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPO ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment