MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemtaka Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) anayekabiliwa na mashitaka ya uchochezi, afike mahakamani leo kujieleza kwa nini asifutiwe dhamana.
Lissu anatakiwa ajieleze kwa sababu yeye a mdhamini wake hawakufika mahakamani jana wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya kutoa uamuzi wa pingamizi la upande wa utetezi.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alitoa amri hiyo jana baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Mutalemwa Kishenyi kuomba Mahakama itoe hati ya kumkamata Lissu kwa sababu ya kutokufika mahakamani.
Awali akitoa uamuzi huo, Hakimu Simba alitupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi na kuruhusu upande wa Jamhuri kuleta upya mashitaka mawili ya uchochezi, ambayo hapo awali yalifutwa kwa kuwa hayakuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Alisema awali mashitaka hayo yaliondolewa kwa sababu hayakuwa na kibali lakini sasa ameyakubali kwa sababu yamewasilishwa pamoja na kibali cha DPP, pia upande wa Jamhuri ulikuwa na haki ya kurekebisha mapungufu na kuyaleta tena mashitaka hayo mahakamani.
Hata hivyo, baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala alidai hawajaridhika, hivyo wanatarajiwa kukata rufaa kuupinga kwa sababu mashitaka hayo yalipofutwa yalikuwa yamekufa.
Aidha, aliiomba Mahakama kutoyasoma mashitaka hayo hadi rufaa yao itakaposikilizwa katika Mahakama Kuu na kutolewa uamuzi. Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekwishakamilika.
Hivi karibuni upande wa utetezi uliwasilisha pingamizi hilo, baada Wakili Kishenyi kuomba kuwasomea washtakiwa hati iliyofanyiwa marekebisho kwa kuongeza mashitaka mawili, ambayo awali yalishafutwa. Katika pingamizi hilo, wakili alipinga washtakiwa hao kusomewa upya mashitaka hayo kwa kuwa mashtaka mapya, hayatofautiani na yale yaliyofutwa mahakamani hapo Juni 28, mwaka huu.
Akijibu hoja hizo, Kishenyi alidai shtaka la kwanza na la tano ni kama hayakuwepo mahakamani na kwamba kuondolewa kwake sheria haikatazi kuyarudisha tena.
Mbali na Lissu washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, mwandishi wa gazeti hilo, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Wanadaiwa kati ya Januari 12 na 14, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa lengo la kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Katika mashtaka yanayomkabili Mehboob, anadaiwa, Januari 13 katika jengo la Jamana, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi, pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
USISAHAU KULIKE NA KU-SHARE NA KU-LIKE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA
ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPO ULIPO.ASANTE
No comments:
Post a Comment