Thursday 1 September 2016

Waziri wa Utalii Profesa Jumanne Maghembe atoa ufafanuzi huu kuhusu hali ya utalii nchini.

Image result for Profesa Jumanne Maghembe
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amesema wizara yake imejiwekea mkazo mkubwa kuhakikisha mchango wa utalii katika Pato la Taifa unafikia asilimia 20 kutoka asilimia 17.5 ya mwaka jana.
 
Kwa mujibu wa Waziri Maghembe, ongezeko la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) halijaathiri sekta hiyo na badala yake mapato yameongezeka.

Amesema, lengo la kuweka mkazo huo ni kuhakikisha robo ya fedha za kigeni zinazoingia nchini zinatokana na pato la utalii na hilo linawezekana kwa kuwa hadi sasa kuna kasi ya ongezeko la watalii nchini.

 Profesa Maghembe alisema wizara imejipanga kutekeleza hilo na kuwa katika msimu huu wa utalii ulioanza wameona matokeo ya kazi ya kutangaza nchi kwenye masuala ya utalii.

“Msimu mkubwa wa utalii umeanza na tumeona matokeo ya kazi tulizofanya, watalii wanaokuja Tanzania mwaka huu ni wengi sasa, mfano kutoka Juni hadi Agosti mwaka huu ukilinganisha na kipindi hiki kwa mwaka jana, kuna ongezeko la asilimia 20 la watalii,” alisema Profesa Maghembe.

Alisema ongezeko hilo sio tu kwa watalii wanaokuja nchini, bali pia limeongeza mapato ya utalii kwa asilimia 22, na kusisitiza kuwa ongezeko la Kodi ya Ongezeko la Thamani inayotozwa kwenye huduma za utalii nchini haijaathiri watalii wanaoingia nchini.

“Ni jambo zuri kuona kuna ongezeko la watalii wanaoingia nchini, lakini pia kuna ongezeko la mapato kwa zaidi ya asilimia 22, licha ya watu kuzungumza matatizo mambo wasiyoyajua vizuri ukweli wake,” amesema Profesa Maghembe.

Akifafanua, alisema mwanzo wa bajeti mpya ya serikali kutangazwa mwaka huu na kuonesha kuwa serikali imeondoa msamaha wa kodi iliyowekwa kwenye sheria ya utalii ya mwaka 2006, ambayo ilisamehe kodi ya ongezeko la thamani kwa huduma zote za utalii.

“Tunaendelea kupinga na kudhibiti biashara na ujangili dhidi ya tembo, kwa sababu tembo wetu wanaisha, walikuwa 110,000 sasa wamepungua chini ya 50,000, wale wote tunaowakamata sasa kwa makosa ya ujangili, tunawashitiaki kwa makosa ya uhujumu uchumi,” amesema.



Alisema kwa mtu yeyote awe mkubwa au mdogo katika vita hiyo hakuna msalia mtume, wote wanaohusika watakamatwa na kushitakiwa. Aliongeza kuwa, kwamba hivi sasa ndege maalumu zisizo na rubani zinazoruka kuangalia wanyama zimesaidia kuongeza ulinzi wa wanyama hao kwa zinapiga picha na kuonesha maeneo waliyoko majangili kisha askari wanafuatilia.

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPO ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment